Marekani na umoja wa Ulaya zaitaka Misri kurejea katika mkondo wa kidemokrasia
8 Agosti 2013Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na mkuu wa sera za nchi za nje wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton, wametoa tangazo la pamoja, wakisema kuwa licha ya ukweli kwamba ghasia zaidi zimeweza kuepukwa, wanao wasiwasi kuhusu mkwamo uliopo kati ya viongozi wa serikali ya mpito na wapinzani wao, katika kupata maridhiano juu ya namna ya kusonga mbele.
Katika tangazo hilo wameongeza kuwa huu ni wakati tete kwa Misri ambao unatishia umwagikaji zaidi wa damu na kuliyumbisha taifa hilo na si hayo tu bali pia inatishia kufufuliwa kwa uchumi wa taifa hilo ambao ni muhimu katika kipindi hiki cha mpito.
Juhudi zaidi zahimizwa
Bi Ashton na Kerry wamesema huu sio muda wa kurushiana lawama bali wakuchukua hatua za kuchochea mazungumzo na kusonga mbele,huku wakisisitiza kuwa Marekani na Umoja huo zitaendelea kuunga mkono nchi hiyo katika kutafuta suluhisho la mkwamo huo wa kisiasa lakini wakasisitiza ni sharti kurejea kwa utawala uliochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
Marekani na umoja wa ulaya zimetoa taarifa ya pamoja kuzihimiza pande zote husika katika mgogoro wa Syria na jeshi lenye nguvu la nchi hiyo kukubaliana kuhusu njia ya kurejea katika utawala wa kidemokrasia.
Juhudi za kidiplomasia za kuutanzua mzozo nchini Misri hazijafua dafu na sasa kuna hofu jeshi huenda likaagiza tena kukabiliwa kwa waandamanaji wanaomuunga mkono Mursi ambao wamekita kambi kwa wiki kadhaa katika maeneo mawili mjini Cairo hadi pale kiongozi huyo atakaporejeshwa madarakani.
Wanadiplomasia washindwa kuwashawishi viongozi
Marekani na Umoja wa Ulaya zilituma wajumbe wao naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani William Burns na mwakilishi maalum wa umoja huo Bernadino Leon nchini humo kufanya mazungumzo na serikali ya muda inayoongozwa na Adly Mansour na viongozi wa udugu wa kiislamu.
Serikali ya muda ya Misri iliyowekwa madarakani mwezi uliopita na jeshi imetaka wafuasi wa Mursi kusitisha maandamano yao na hivyo kuzua hofu kuwa huenda kukaibuka tena ghasia.
Utawala wa Mansour ulighadhabishwa mapema wiki hii na matamshi ya seneta wa Marekani John McCain aliyeizuru nchi hiyo kwa kusema kuondolewa madarakani kwa Mursi hakuna jina jingine bali ni mapinduzi ya kijeshi.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Jay Psaki amesema matamshi hayo ya McCain hayawakalishi msimamo wa Marekani.
Mwandishi:Caro Robi/afp/reuters
Mhariri. Gakuba Daniel