Marekani na Uingereza zamuonya Assad
23 Agosti 2012Katika mazungumzo yao kwa njia ya simu, viongozi hao wamekubaliana kwamba " kutumia au kutishia kutumika kwa silaha za kemikali ni jambo lisilikubalika na kutawalazimisha wao kuchukua hatua mapema".
Wote kwa pamoja wamesema wanataka kuona upinzani wenye kuaminika na kutumaini kwamba katika mkutano ujao huko Misri utaonesha mshikamano wa kweli na mfungamano katika kuelekea kufanya kazi pamoja kuelekea serikali ya mpito.
Ikulu ya Marekani imesema Obama alionesha wasiwasi kwa Comeron kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria, na kutoa wito kwa mataifa tofauti kutoa misaada yao kupitia Umoja wa Mataifa.
Taarifa hiyo inasema viongozi wote wawili walibadilishana mawazo juu ya namna jumuiya ya kimataifa inavyoweza kulisaidia taifa hilo na kufanikisha shinikizo zaidi kwa rais Bashar al Assad kuondoka madarakani.
Cameron, ambae amerudi hivi punde baada ya mapunziko mafupi ya msimu wa kiangazi, amezungumza kwa wakati tofauti na rais Francois Hollande ambae anataka Syria itupiwe jicho kwa ukaribu zaidi.
Nchini Syria kwenyewe majeshi ya serikali ya taifa hilo yanakabiliana vikali na waasi katika jiji la Damascus. Kwa mujibu wa wanaharakati, mashambulio yanafanyika katika wilaya kadhaa za mji huo kwa kuziripua baadhi ya nyumba.
Ndege za kivita pamoja na vifaru vimeripotiwa kushambulia maeneo yanayokaliwa na waasi, huko katika mji wa kaskazini wa Aleppo ambapo makundi ya wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kwamba raia wanakabiliwa na hali mbaya sana ya kiutu.
Kiasi ya watu 15 wameripotiwa kuuwawa na wengine 150 wamejeruhiwa katika kitongoji cha Daraya, kilichopo kusini/magharibi mwa Syria. Chanzo kimoja kilisema vikosi vimekuwa vikiendesha operesheni ya nyumba kwa nyumba katika makazi ya Waislam wa madhehebu ya Sunni.
Jana kiasi ya watu 41 wameripotiwa kuuwawa Damascus pekee ambapo pamoja na askari wa nchi kavu, helikopta na vifaru vilitumika pia katika kufanikisha mashambulio hayo. Wanaharakati wanasema ilikuwa ni moja kati operesheni mbaya zaidi kufanyika katika eneo hilo tangu majeshi ya serikali kudai kuudhibiti mji huo takribani mwezi mmoja uliyopita.
Taarifa makundi ya waangalizi zinasema takwimu za jana zinaonesha watu 167, wakijumuishwa raia 71, wameuwawa katika maeneo tofauti ya taifa hilo jana pekee. Idadi hiyo inaafanya idadi ya watu waliuwawa kufikia watu 23,000 tangu kuanza kwa vurugu hizo Machi 2011. Lakini Umoja wa Mataifa unasema watu 17,000 ndio waliuwawa.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Miraji Othman