1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Miaka 50 ya Makubaliano ya Rome Magazetini

Oumilkheir Hamidou
14 Desemba 2016

Mwelekeo wa siasa za siku za mbele za Marekani ulimwenguni, Umoja wa Ulaya, na miaka 50 tangu yalipotiwa saini makubaliano ya Roma ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/2UFLY
Symbolbild US-Wahl - Donald Trump & Wladimir Putin
Picha: picture-alliance/dpa/S. Thew & A. Druzhinin/Ria Novosti/Kremlin Pool

Tunaanzia Marekani ambako walimwengu wanafuatilizia kwa makini mwelekeo anaopanga kuufuata rais mteule Donald Trump. "Matajiri,majenerali na wanaume" ndio watakaomata nafasi muhimu katika serikali mpya ya Marekani. Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:

Mwongozo wa siasa za siku za mbele za Marekani huenda usieleweke,haimaanishi lakini kuwa hali itaendelea kuwa hivyo. Kilicho na uhakika ni kwamba kwa kuingia madarakani Donald Trump, mtindo mpya wa kisiasa utaanza ikulu ya White House. Hali hiyo inadhihirishwa na wale aliowateuwa; wahafidhina waliobobea, madume na matajiri; sifa zinazolingana na wengi kati ya wanachama walioteuliwa katika kundi la Trump. Hakuna ishara lakini ya kuendelezwa sera za haki katika jamii, afya au mazingira zilizokuwa zikifuatwa wakati wa enzi za Obama. Mengi yatadurusiwa-ikiwa ni pamoja na uhusiano pamoja na Urusi unaobidi kurekebishwa na angalao suala hilo linatia moyo."

Ufumbuzi wa mizozo ya dunia utapatikana kwa ushirikiano pamoja na Urusi

Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linajishughulisha zaidi na athari za kuelemea mrengo wa kushoto serikali mpya ya Marekani. Gazeti linaendelea kuandika: "Trump anaielekeza siasa ya Marekani mrengo wa kushoto; na zaidi kuliko yote anajaribu kuijongelea Urusi. Kwasababu Rex Tillerson anatajwa kuwa rafiki mkubwa wa Vladimir Putin. Lakini uamuzi wake unamaanisha nini kwa siasa ya kimataifa? Kitatokea kipi tajiri anaemiliki kampuni la mafuta, atakapopanda jukwaa la kisiasa? Anaweza pengine angalao kusawazisha uhusiano uliodhoofika pamoja na Urusi. Na wakati ndio huu: Kwa sababu kimoja kimebainika: bila ya kiongozi wa Urusi, mizozo mingi duniani haiwezi kutatuliwa; Vita vya Syria, mzozo wa Ukraine, mipango ya kujipanua jumuia ya kujihami ya NATO kuelekea mashariki ya Ulaya-orodha ya majukumu ni ndefu. Tillerson anabebeshwa matumaini tu , hakuna la ziada."

Miaka 50 ya makubaliano ya Roma

 Mada yetu ya pili magazetini inahusu mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa ulaya utakaoitishwa kesho mjini Brussels. Gazeti la "Mittelbayerische" linazungumzia hofu zinazojitokeza kutokana na jinsi fikra ya kuundwa Umoja huo inavyoangaliwa katika baadhi ya nchi. Gazeti linaendelea kuandika: "Viongozi wa serikali za Ulaya hawatambuani. Miaka takriban 50 iliyopita, baada ya kutiwa saini makubaliano ya Rome, maandalizi ya sherehe za maadhimisho hayo yanaendelea kwa kasi mjini Rome ambapo mwezi March mwakani viongozi wanatarajiwa kusifu mradi wa amani katika hotuba zao pamoja na kuonya dhidi ya kuvurugwa yaliyofikiwa na  kuwatahadharisha vijana wasipuuze yaliyofikiwa. Mbali na sherehe hizo viongozi wanatambua jinsi raia wa Umoja wa ulaya wanavyozidi kupuuza yaliyofikiwa. Nchini Uingereza walikuwa wazee waliopiga kura nchi hiyo itoke katika Umoja wa ulaya. Nchini Italy vijana ndio wanao upa kisogo Umoja wa ulaya na kujiunga na makundi  yanayoupinga umoja huo mfano wa vuguvugu la nyota tano.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir

Mhariri: Grace Patricia Kabogo