1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Korea Kusini zaanza mazoezi ya kijeshi

Yusra Buwayhid
21 Agosti 2017

Wanajeshi wa Marekani na Korea Kusini wameanza mazoezi ya kijeshi ya kila mwaka, baada ya Rais Donald Trump na Kim Jong Un kujibizana maneno ya kuashiria vita na majaribio mawili ya makombora ya Korea Kaskazini.

https://p.dw.com/p/2iY1A
Südkorea Gemeinsame Militärübung mit der USA
Picha: Getty Images/AFP/Jung Yeon-Je

Mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka yajulikanayo kama 'Ulchi Freedom Guardian' ambayo kwa kiasi kikubwa yanaendeshwa kwa kompyuta kwa teknolojia ya kidijitali na kufanyika kila majira ya joto, yamepokewa kwa hasira na upande wa Korea Kaskazini, ambayo inayatazama kama mazoezi ya kujitayarisha kwa uvamizi.

Akizungumza na Baraza lake la mawaziri, Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in, amesema leo  kwamba ushirikiano wa kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani haukusudii kuongeza mvutano kwenye rasi ya Korea, na ameionya Korea Kaskazini dhidi ya kulitumia zoezi hilo la kijeshi kama sababu ya kufanya vitendo vya uchochezi.

"Korea Kaskazini inapaswa kufahamu kwamba kutokana na uchokozi wake wa mara kwa mara, zoezi la pamoja kati ya Korea Kusini na Marekani litaendelea. Natumai kuwa maafisa wa serikali zetu pamoja na wanajeshi wapo tayari kujibu uchokozi wowote ule utakaotokana na zoezi la mara hii, na nawataka watu wetu kuwa na mshikamano zaidi kuliko wakati mwengine wowote," amesema Rais, Moon Jae-in, wa Korea Kusini.

Südkorea Präsident Moon Jae-in
Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-inPicha: Getty Images/Jeon Heon-Kyun-Pool

Korea Kaskazini hujibu kwa majaribio ya makombora

Kawaida Korea Kaskazi hujibu mazoezi hayo ya kijeshi kwa majaribio ya silaha na msururu wa maneno ya ugomvi. Wakati wa mazoezi ya mwaka jana, Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kurusha kombora la masafa marefu kutoka katika manowari, ambalo liliruka umbali wa kilomita 500 ikiwa ni masafa marefu zaidi kwa silaha ya aina hiyo. Siku kadhaa baada ya mazoezi hayo ya kijeshi, Korea Kaskazini ilifanya jaribio lake la tano la kinyuklia na kubwa zaidi kuwahi kutokea hadi hii leo.

Licha ya vitisho kutoka Korea Kaskazini, Marekani na Korea Kusini leo zimezindua mazoezi yake ya kijeshi ya siku 11. Mazoezi hayo yanajumuisha wanajeshi 17,500 wa Kimarekani, na wanajeshi wengine 50,000 kutoka Korea Kusini, kulingana na makamanda wa kijeshi wa pande zote mbili pamoja na taarifa za Wizara ya Ulinzi ya Seoul.

Huku hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, amesema haoni kama Ujerumani ina jukumu la upatanishi katika mzozo huo wa rasi ya Korea kuhusu mpango wa kinyuklia wa Korea Kasakazini. Lakini amesema kwamba Umoja wa Ulaya unaweza ya ukatoa utaalamu wake ulioupata katika kuongoza mazungumzo yaliyofikia makubaliano ya mpango wa kinyuklia wa Iran ya mwaka 2015.

Ujerumani hata hivyo ni moja ya nchi chache zilizo na ubalozi wake Korea Kaskazini katika mji mkuu wa Pyongyang.

 

Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa/ap

Mhariri:Josephat Charo