1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Korea Kusini wafanya mazoezi makubwa ya kijeshi

4 Desemba 2017

Mazoezi hayo ya kila mwaka yanajiri siku tano tu, baada ya Korea Kaskazini kufyatua kombora lake la masafa marefu, lenye nguvu zaidi na ambalo linaweza kufika sehemu yoyote nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/2oiF3
Südkorea und USA beginnen Luftwaffenübung
Picha: Reuters/News1/Oh Jang-hwan

Marekani na Korea Kusini zimeanza mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya angani. Mazoezi hayo ndiyo makubwa zaidi kuwahi kufanywa na nchi hizo. Korea Kaskazini imeyataja mazoezi hayo kuwa ni uchokozi wa wazi.

Mazoezi hayo ya kila mwaka yanajiri siku tano tu, baada ya Korea Kaskazini kufyatua kombora lake la masafa marefu, lenye nguvu zaidi na ambalo linaweza kufika sehemu yoyote nchini Marekani.

Kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini, mazoezi hayo ya angani yatakayodumu kwa siku tano, na ambayo yameanza leo, yanajumuisha jumla ya ndege 230, zikiwemo ndege za kivita aina ya F-22 Raptor Stealth Fighters, na maelfu ya wanajeshi.

Akithibitisha kuanza kwa mazoezi hayo, Moon Sang-Gyun ambaye ni msemaji wa jeshi la Korea Kusini amesema: "Jeshi la angani la Korea Kusini pamoja na kikosi cha saba cha jeshi la angani la Marekani, yatafanya mazoezi maalum ya tahadhari kuanzia leo hadi Disemba nane ili kuimarisha uwezo wa kivita wa  pamoja wa majeshi ya angani ya Korea Kusini na Marekani."

Jumla ya ndege 230 zinajumuishwa katika mazoezi hayo
Jumla ya ndege 230 zinajumuishwa katika mazoezi hayoPicha: picture-alliance/AP Photo/Yonhap

Korea Kaskazini imeshutumu juu ya hatua hiyo na kuukosoa utawala wa Donald Trump kwa kile ilichosema ni kutafuta vita vya kinyuklia.

Japan: Majaribio ya Korea kaskazini ni kitisho kwa Japan

Bunge la Japan limesema majaribio ya makombora yanayofanywa na Korea Kaskazini ni kitisho kikubwa kwa nchi yake. Wakati huo huo waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema hakuna sababu ya  kuzungumza na taifa kaidi la Korea Kaskazini.

Bunge la Japan limepitisha kauli ya kuishutumu Korea Kaskazini kwa kufyatua kombora la kutoka bara moja hadi jingine wiki iliyopita ambalo lilianguka baharini ndani ya mipaka ya kiuchumi ya Japan.  Hatua hiyo ilidhihirisha nia ya Korea Kaskazini kuendelea na mipango yake ya nyuklia na makombora.

Picha inayoonesha kombora la masafa marefu lililofanyiwa majaribio Julai 28, 2017
Picha inayoonesha kombora la masafa marefu lililofanyiwa majaribio Julai 28, 2017Picha: Getty Images/AFP/KCNA

Lindsey Graham: Marekani yasogea karibu katika vita na Korea Kaskazini

Hali ya wasiwasi ikiendelea kutokota, seneta mwenye ushawishi mkubwa kutoka chama cha Republic nchini Marekani na ambaye ni mchambuzi wa sera za kimataifa, Lindsey Graham ameonya kuwa Marekani inasogea karibu katika vita na Korea Kaskazini. Amekiambia kituo cha televisheni cha CBS kuwa ikiwa Korea Kaskazini itafanya jaribio la kombora la ardhini, basi Korea Kaskazini inapaswa kujiandaa kupata jibu kali kutoka Marekani.

Korea Kaskazini imejigamba kuwa kombora aina ya Hwasong 15 lililofanyiwa majaribio wiki iliyopita lina uwezo wa kufikisha kichwa kikubwa cha nyuklia mahali popote ndani ya Marekani.

Wachambuzi wamekiri kuwa jaribio hilo la hivi karibuni linaonesha hatua kubwa iliyopigwa na Korea Kaskazini kuwezesha makombora yake kufika mbali zaidi, lakini wanasema liliwezeshwa kwa kutumia kichwa bandia cha nyuklia ambacho ni chepesi sana.

Mwanadhishi: John Juma/AFPE

Mhariri:Yusuf Saumu