1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Japan kuamua nani bingwa wa dunia

16 Julai 2011

Bingwa wa kombe la dunia kwa kandanda la wanawake atajulikana rasmi Jumapili, wakati Marekani na Japan watakapokipiga kuwania taji hilo. Wakati huo huo Ufaransa na Sweden wanawania medali ya shaba.

https://p.dw.com/p/11wSJ
Kushoto ni timu ya wanawake wa Marekani na kulia ni timu ya Japan. Timu hizo zinakumbana katika fainali kesho .Picha: AP/DW-Fotomontage

Baada ya kushindwa katika mchezo wa nusu fainali, Sweden sasa inakumbana na Ufaransa kuwania nafasi ya tatu leo Jumamosi , wakati kesho Jumapili bingwa wa kombe la dunia kwa wanawake atafahamika wakati Marekani ina miadi na Japan.Katika kombe la Copa America , Uruguay bingwa mara 14 wa kombe hilo inawania kusonga mbele katika nusu fainali leo itakapotiana kifuani na Argentina.

Nae bingwa wa dunia wa mbio za mita 10,000 kutoka Kenya Linet Maasai anamatumaini ya kukamilisha ubingwa mara mbili mwezi ujao katika mashindamo ya riadha ya dunia mjini Daegu Korea ya kusini.

Baada ya kupoteza mchezo wa nusu fainali katika kombe la dunia kwa wanawake , Sweden inapambana na Ufaransa leo Jumamosi katika kuwania nafasi ya tatu, huku pande zote hizo mbili zikisisitiza kuwa zinaitaka medali hiyo ya shaba. Sweden ilichapwa mabao 3-1 na Japan mjini Frankfurt siku ya Jumatano, na usiku huo huo Ufaransa ikaonja joto ya jiwe baada ya kukandikwa nayo mabao 3-1 na Marekani mjini Moenchengladbach. Wakati Japan na Marekani zinajiwinda kulinyakua taji la ubingwa wa dunia kwa wanawake siku ya Jumapili , Wafaransa na Waswidi watapambana baada ya kupata nafasi mbili zilizowazi katika michezo ya mwaka 2012 ya Olimpiki mjini London kwa kufika kwao katika nusu fainali.

Baada ya kikosi cha Sweden kudhibitiwa vilivyo na Japan , kocha wa Sweden Thomas Dennerby alielezea kwa nini aliwaita wachezaji wake katikati ya uwanja mjini Frankfurt na kuwataka wapeleke nguvu zao katika kumalizia kampeni yao kwa ushindi leo jioni.

Marekani inakabiliana na Japan kesho Jumapili wakitafuta ushindi wa tatu wa kombe la dunia, na wakati mbinu na ubunifu zimechukua nafasi ya juu katika mchezo wao na kuwafikisha katika fainali , ni hali ya kujisikia kuwa huru na shauku ambayo timu hiyo inayo, ambayo ndio iliyowaletea mafanikio mara hii katika michezo hiyo hapa Ujerumani. Katika michezo miwili iliyopita , Marekani imeweza kuzishinda timu mbili, Ufaransa na Brazil , ambapo wachunguzi wengi wa masuala ya soka wanaamini zilikuwa zenye mbinu na wachezaji wenye vipaji kuliko Marekani. Lakini kocha wa timu hiyo Sundhage amesema ni kutokana na bidii waliyonayo wachezaji wake. Nahodha wa timu ya Marekani kuhusu mchezo wa fainali hapo kesho anasema.

"Kucheza katika fainali katika mashindano yoyote ni jambo la kusisimua, kila mara ni heshima yenye fadhila kubwa. Huwezi kufikia katika kiwango hicho na mchezaji mmoja, kichwa kimoja, huwezi kufikia hapo kwa mara moja. Kwetu sisi ilikuwa ni juhudi za pamoja kwa kila mtu aliyehusika, sio tu wachezaji lakini hata wasaidizi wetu wote".

Japan nayo imefanikiwa kufikia lengo lao. Katika mchezo ya nusu fainali timu hiyo ilipata tena ushindi. Japan ilikuwa jinamizi kwa Ujerumani timu ambayo ilikuwa inaota ndoto ya kulitwaa kombe la dunia la wanawake kwa mara ya tatu mfululizo, kwa kuichapa bao 1-0 katika dakika za nyongeza , lakini pia haikuwapa nafasi Sweden kutamba dimbani. Iliipa kipigo cha mbwa mwizi Sweden kwa kuitandika mabao 3-1. Mashabiki wa Japan wakifurahia ushindi huo walikuwa na haya ya kusema.

"Safi sana , walifanya vizuri sana na walikuwa na nafasi nyingi za kufunga lakini tulitumia nafasi tulizopata vizuri".

"Wachezaji wa Japan walicheza vizuri sana, sikutegemea hilo. Wasweden walikuwa ndio wanaotarajiwa kushinda , hata hivyo".

Timu ya mpira wa miguu ya wanawake wa Japan inacheza kwa ajili ya nchi yao na wanaonyesha hivyo kila baada ya mchezo. Kuwa na matumaini ndio nguzo yao kubwa ya kupata motisha.

Na kwa upande wa kombe la Copa America , Uruguay ina miadi na Argentina katika mchezo mkali wa robo fainali hii leo jioni. Timu hizo hasimu , ambazo zinashikilia rekodi ya kulinyakua kombe hilo mara 14 kila mmoja, zinapambana katika kile kinachojulikana kama Clasico del Rio de la Plata, mjini Santa Fe leo Jumamosi usiku , ambapo timu zote mbili zinataka kunyanyua kiwango cha mchezo wake. Argentina ilirekebisha mchezo wake katika kundi A wakati ilipoichapa Costa Rica mabao 3-0, Lionel Messi akikaribia kiwango chake cha juu cha kusakata soka , lakini hadi sasa hajauweka mpira wavuni, katika michezo 15 iliyopita ya nchi yake. Lakini kocha wa Uruguay amesema kujaribu kumuwekea mtu wa kumlinda Lionel Messi hakutaisaidia timu yake, isipokuwa Uruguay inapaswa kujiamini na kile inachokiweza. Ikiwa unatatizo na huna jibu lake , kwa nini ujitie mashakani. Messi anaweza kutupatisha taabu na hili halitaondoka hata tufanye nini , amesema Tabarez mjini Buenos Aires. Lakini kuna mengi ambayo tunayaweza , ambayo si Messi ama mtu yeyote anaweza kuyazuwia, mambo hayo ni sehemu ya utambulisho wetu, utambulisho wa timu ya Uruguay, ambayo ni tabia ya ubishi, ukakamavu, na kujiamini kwamba tunaweza. Hayo ni mambo tunayoyaweza, amesema Tabarez.

Fußball WM 2010 Deutschland Argentinien
Timu ya taifa ya Argentina, mbele kulia anaonekana Lionel MessiPicha: AP

nayo Peru , ikiwa na ndoto ya kupata ushindi kwa mara ya kwanza katika miaka 36, itajaribu kuizuwia Colombia leo katika mpambano wao wa copa America katika robo fainali nyingine. Tunakabiliana na Colombia. Ni kibarua kigumu, lakini tunapaswa kuwa na imani kwamba tunaweza kuwaondoa. Songa mbele Peru, anasema mshambuliaji wa Peru , Paulo Guerrero, ambaye anaichezea timu ya Bundesliga nchini Ujerumani ya Hamburg, katika ukurasa wake wa twita. Mpambano wa hivi karibuni baina ya timu hizo ulikuwa mgumu, na kuishia na sare ya bao 1-1 mjini Bogota katika mchezo wa kirafiki Novemba mwaka jana pamoja na mchezo wa kuwania kukata tikiti ya kombe la dunia ambapo uliishia kwa ushindi wa bao 1-0 kwa Colombia na bao 1-1 nyumbani nchini Peru.

AS Roma inaanza enzi mpya kwa kucheza aina ya soka inayochezwa na Barcelona ya Hispania , amesema kocha mpya wa klabu hiyo ya Serie A Luis Enrique wakati akitambulishwa rasmi wiki hii. Mhispania huyo ambaye aliwahi kukifunza kikosi B cha timu ya Barcelona kabla ya kuchukua nafasi ya Vincenzo Montella mwezi uliopita, amesema lengo lake ni kujenga kikosi cha vijana wadogo, kitakachojengwa kutokana na maadili. wakati nikizungumza na uongozi wa AS Roma kuhusu mkataba wangu , waliniambia wazo lilikuwa ni kuwa na kikosi kitakachosakata soka la kufurahisha, tutaangalia baada ya miezi michache ijayo iwapo tutafanikisha hilo, lakini sifahamu njia nyingine ya kucheza soka. Nae mmiliki mpya wa klabu hiyo ya Roma Di Benedetto amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa wavumilivu wakati kocha mpya Luis Enrique anaijenga enzi mpya ya klabu hiyo.

Kocha mkuu wa Arsenal London Arsene Wenger amewataka wachezaji wa Barcelona kuacha kutoa matamshi hadharani juu ya nahodha wa timu hiyo Cesc Fabregas kwenda kuichezea klabu hiyo ya Nou camp. Kocha huyo Mfaransa alikuwa akizungumza baada ya mchezaji wa kiungo wa Barcelona Xavi kusema kuwa Fabregas hana raha na anataka kurejea katika klabu anayoishabikia toka utotoni mwake. Frabregas amebakia mjini London wakati akipona maumivu ya msuli. Wenger na timu yake walilakiwa na mamia ya mashabiki waliovalia jezi nyekundu wakati mamia kwa maelfu ya mashabiki walipojitokeza kuwalaki wakati wakianza ziara yao nchini China katika muda wa miaka 16.

Arsene Wenger
Kocha mkuu wa Arsenal London , Arsene Wenger amewaonya wachezaji wa Barcelona kutozungumza kuhusu Fabregas.Picha: picture-alliance/ dpa

Nae mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia Radamel Falcao amekataa nafasi ya kujiunga na vigogo wa soka katika bara la Ulaya kwa kurefusha mkataba wake na Porto hadi mwaka 2015, mabingwa hao wa Ureno wametangaza Alhamis wiki hii.

Kwa upande wa riadha Mkenya Linet Maasai bingwa wa dunia wa mbio za mita 10,000 amesema wiki hii kuwa anamatumaini ya kukamilisha ushindi mara ya pili katika mashindano ya dunia ya mwezi ujao mjini Daegu nchini Korea ya kusini. Akihakikishiwa kuwa na nafasi yake katika mbio za mita 10,000, Maasai ameongeza kasi ya kampeni yake ili kuchaguliwa kukimbia mbio za mita 5,000 pia katika mashindano hayo ya dunia, wakati aliposhinda bila kizuwizi mbio zake za nusu fainali mwanzoni mwa fainali za majaribio nchini Kenya wiki hii.

Na kwa taarifa hiyo mpendwa msikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kuwaletea kipindi hiki cha michezo kwa leo, jina langu ni Sekione Kitojo , hadi mara nyingine , Kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre /afpe

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman