1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Iran zaashiria kupunguza mvutano

Daniel Gakuba
9 Januari 2020

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema nchi yake iko tayari kuzungumza na Iran bila masharti, katika juhudi za kutuliza mvutano ulioshamiri baada ya Marekani kumuuwa jenerali maarufu wa Iran, Qasem Soleimani.

https://p.dw.com/p/3Vvf4
Golf Iran Soleimani
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. D. Josek

Maelezo ya Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yamewasilishwa katika barua iliyotumwa jana na balozi wake, Kelly Craft, ambapo amesema shambulizi la anga lililomuuwa jenerali Soleimani liliheshimu kipengele nambari 51 cha mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinasisitiza haki ya kila nchi mwanachama kujilinda ikiwa itashambuliwa kwa silaha.

Amesema mnamo miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Marekani na maslahi ya nchi hiyo katika Ukanda wa Mashariki ya Kati vimekuwa vikishambuliwa mara kwa mara na Iran pamoja na makundi ya wanamgambo yanayoiunga mkono.

Mazungumzo bila masharti

Hata hivyo, balozi huyo ameongeza kuwa Marekani iko tayari kuzungumza na Iran bila masharti, kwa nia ya kuepusha kitisho kwa usalama wa kimataifa, pamoja na kupanuka kwa mzozo kati ya nchi hizo zenye uhasama wa miongo mingi.

USA Washington Weißes Haus | Donald Trump, Präsident | Statement Iran
Rais Donald Trump akilihutubia taifa baada ya kambi zake nchini Iraq kushambuliwa na IranPicha: AFP/S. Loeb

Katika hotuba ya rais wa Marekani Donald Trump jana jioni, ya kwanza baada ya Iran kulipiza kisasi mauaji ya Jenerali Qasem Soleimani kwa kuvilenga vituo vya jeshi la Marekani nchini Iraq, rais huyo alitoa ishara ya kutuliza joto katika mvutano uliotishia vita kamili kati ya nchi hizo.

Alisema inaelekea Iran wamepunguza uhasama, akiongeza hiyo ni habari njema kwa wote wanaotaka amani kwa mashariki ya kati.

Iran nayo yajieleza

Kwa upande wake, Iran nayo ililiarifu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusu ilichokitaja kuwa 'hatua za kadri za kulipiza kisasi' dhidi ya Marekani, kwa mauaji ya jenerali Soleimani.

Iranische Fateh-110 Boden-Boden-Rakete
Kombora chapa Fateh-110 lililotumiwa na Iran kuzihambulia kambi za jeshi la Marekani nchini IraqPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Reza Alaei

Katika barua iliyowasilishwa na balozi wake katika umoja huo, Majid Takht Ravanchi, ilielezwa kuwa shambulizi la makombora lililofanywa na Iran usiku wa kuamkia jana dhidi ya vituo viwili vya jeshi la Marekani nchini Iraq, lilichukuwa tahadhari ya kuepusha hasara kwa miundombinu ya kiraia.

Hata hivyo, balozi Ravanchi alitilia shaka azma ya Marekani ya kulegeza kamba ya uhasama wake dhidi ya Iran, wakati huo huo ikitangaza vikwazo vipya vya kiuchumi. Katika barua yake barua huyo alisisitiza kwa mara nyingine kwamba Iran iko tayari kulinda watu wake na himaya yake dhidi ya uvamizi wowote.

Saa chache baada ya hotuba ya rais Trump jana jioni, eneo uliko ubalozi wa Marekani mjini Baghdad lilishambuliwa kwa maroketi mawili, na waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper alisema wanatarajia mashambulizi kama hayo kutoka kwa makundi ya wanamgambo wa kishia.

RTRE, APE