1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na China waanza raundi mpya ya mazungumzo

28 Machi 2019

Marekani na China wameana awamu nyingine ya majadiliano ya kibiashara wakati ambapo mataifa hayo makubwa yakikaribia kupata muafaka wa mzozo wa kibiashara uliodumu kwa miezi kadhaa baina yao. 

https://p.dw.com/p/3FpSm
USA Handelsgespräche mit China in Washington | Lighthizer & Mnuchin & Ross & Liu He
Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

 

China imesema wanaohusika katika mazungumzo hayo bado wana kazi kubwa ya kufanya mbele yao wakati wanapokutana kwa ajili ya majadiliano hayo mapya yanayolenga kutafuta suluhisho la vita vya kibiashara kati yao.

Mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer pamoja na waziri wake wa fedha Steven Munuchin wamekwishawasili Beijing tayari kwa ajili ya mazungumzo hayo ya siku mbili, pamoja na mwanauchumi wa ngazi za juu wa China Liu He.

Awali msemaji wa wizara ya biashara ya China Gao Feng amesema kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Beijing kwamba Liu, Mnuchin na Lighthizer wamepiga hatua kubwa baada ya kuwasiliana mara kadhaa kwa njia ya simu.

Alisema "Pande zote mbili zimepiga hatua kubwa, lakini bado kuna kazi ya kufanywa. Ujumbe wa Marekani utawasili baadae mchana huu na watakuwa na mkutano wakati wa chakula cha jioni, lakini pia wataitumia siku nzima ya kesho kujadiliana. Wiki ijayo, makamu wa waziri mkuu Liu He atazuru washington na kuwa na awamu ya tisa ya mazungumzo na wawakilishi wa ngazi za juu wa Marekani na China kuhusu masuala ya biashara na uchumi".

Robert Lighthizer, Steven Mnuchin, Xi Jinping
Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin akipeana mkono na rais wa China Xi Jinping. Pembeni yao ni mwakilishi wa biashara wa Marekani, Robert LighthizerPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Wong

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin ameelezea matumaini yake kwenye mazungumzo hayo akisema pande zote mbili zitajadiliana kwa uwazi na yenye manufaa hasa kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya rais Xi Jinping wa China na Donald Trump wa Marekani mnamo mwezi Disemba. Amesema, iwapo hakutafikiwa makubaliano kwa sasa, watatafuta mpango mwingine.

Makamu wa rais wa baraza la biashara la pamoja la China na Marekani, Jacob Parker amesema washiriki wa majadiliano hayo wanatarajia kuondoa tofauti zilizosalia kwenye masuala kadhaa, lakini kubwa ni kuhusu ruzuku ya China kwa makampuni inayoelezwa na Marekani inaondoa fursa sawa baina ya makampuni ya ndani na ya nje. 

Ingawa rais Trump ana matarajio makubwa ya kufikia makubaliano hivi karibuni, lakini kuendelea kwa majadiliano hayo kunamaanisha kwamba bado kuna tofauti za msingi baina yao.

Marekani na China zimekuwa katika vita vya kibiashara na kuwekeana ushuru wa mabilioni ya dola kwenye bidhaa tangu mwaka jana na kuwaathiri kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara. Trump, wiki iliyopita alishauri ushuru huo uendelee kuwepo hata baada ya makubaliano ili kuhakikisha China inatekeleza masharti ya Marekani.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/APE

Mhariri: Gakuba, Daniel