1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Afrika Kusini zakubaliana kufanya mageuzi Zimbabwe

Kabogo Grace Patricia7 Agosti 2009

Makubaliano hayo yamefikiwa leo kati ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani na mwenzake wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane.

https://p.dw.com/p/J5jN
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: AP

Marekani na Afrika Kusini zimekubaliana kufanya juhudi za pamoja kubadilisha demokrasia, uhuru na ustawi wa Zimbabwe. Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Pretoria uliohudhuriwa pia na Wanziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane.

Bibi Clinton amesema nchi hizo mbili zinafanya kazi pamoja kuhakikisha kuwa mfumo wa kidemokrasia wa Zimbabwe unafanyiwa mageuzi. Ahadi hiyo ya kufanya kazi pamoja inaonyesha dalili nzuri baina ya Marekani na Afrika Kusini, baada ya kutokuwepo mahusiano mazuri katika miaka ya hivi karibuni wakati wa utawala wa Thabo Mbeki, kutokana na makubaliano ya Zimbabwe, kupiga vita ugonjwa wa Ukimwi na kitendo cha Marekani kuivamia Iraq.

Marekani imekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, huku ikishinikiza kufanyika mageuzi kadhaa chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo waziri wake mkuu, Morgan Tsvangirai, ni kiongozi wa zamani wa upinzani. Kwa pamoja Marekani na Umoja wa Ulaya zimemuwekea Rais Mugabe vizuizi vya kusafiri kwenda katika nchi hizo na kutaka kuzuiwa kwa mali zake.

Bibi Clinton amesema kuwa wanakusudia kuwalenga viongozi wa Zimbabwe kwa kuwawekea vikwazo ambavyo havitawaathiri wananchi wake. Ameongeza kuwa kabla ya vikwazo hivyo havijaondolewa na kuruhusu kupelekwa kwa misaada, Marekani inataka kuona kuwa Zimbabwe inafanya mageuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Waziri huyo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, amesema kuwa Afrika Kusini inafahamu vizuri changamoto zilizosababishwa na mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe, kwa sababu Afrika Kusini ina wakimbizi milioni 3 wa Zimbabwe. Msimamo wa rais mpya wa Afrika Kusini, Jacob Zuma umeonyesha matumaini ya kuwepo kwa uhusiano imara baina ya nchi hizo mbili na Bibi Clinton kesho anatarajia kukutana na Rais Zuma.

Aidha, Bibi Clinton amesema kuwa Rais Barack Obama wa Marekani, amekuwa na hamu kubwa ya kufanya kazi kwa karibu na Zuma pamoja na Afrika Kusini kwa ujumla. Akizungumzia uhusiano uliopita baina ya utawala wa George W. Bush na Mbeki, Waziri Nkoana-Mashabane, amesema kuwa nchi hizo zimekubaliana kuimarisha uhusiano wao katika masuala mbalimbali kitu ambacho hakikufanyika miaka minane iliyopita.

Baadaye leo, Bibi Clinton atamtembelea Rais wa Zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na kutembelea kituo cha mradi wa Ukimwi. Bibi Clinton yuko Afrika Kusini katika kituo chake cha pili cha ziara yake ya mataifa saba ya Afrika akitokea nchini Kenya na anatarajiwa kuondoka nchini humo keshokutwa Jumapili, na kuendelea na ziara yake katika nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Nigeria, Liberia na Cape Verde. Ziara hii ya siku 11 ni ziara ndefu kufanywa na Bibi Clinton tangu achaguliwe kushika wadhifa wake huo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFP/RTRE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman