1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutathmini ushirikiano wa kijasusi na Ujerumani!

23 Mei 2015

Serikali ya Ujerumani imekataa kuzungumzia repoti kwamba mashirika ya ujasusi ya Marekani yanatathmini upya ushirikiano wao na wenzao wa Ujerumani na imesitisha miradi ya pamoja kutokana na kuvujishwa taarifa za siri.

https://p.dw.com/p/1FVUm
Nembo ya shirika la ujasusi la Ujerumani BND (kushoto) na shirika la usalama wa taifa la Marekani (kulia).
Nembo ya shirika la ujasusi la Ujerumani BND (kushoto) na shirika la usalama wa taifa la Marekani (kulia).Picha: imago

Gazeti la Bild limeripoti Jumamosi (23.05.2015) kwamba mkuu wa shughuli za upelelezi nchini Marekani James Clapper ameamuru kufanyika kwa tathmini hiyo kwa sababu nyaraka za siri kuhusu uhusiano wa shirika la ujasusi la Ujerumani BND na Marekani zilivujishwa kwa vyombo vya habari na kamati ya bunge la Ujerumani.

Msemaji wa ubalozi wa Marekani mjini Berlin amesema ubalozi huo hauzungumzii masuala ya ujasusi.

Madai kwamba shirika la ujasusi la Ujerumani BND liliisaidia Shirika la Usalama la Taifa nchini Marekani (NSA) kuzifanyia upelelezi kampuni za Ulaya na maafisa wa serikali zimekuwa zikigonga vichwa vya habari kwa wiki kadhaa nchini Ujerumani na kuiweka katika hali ya mashaka serikali ya mseto ya Kansela Angela Merkel pamoja na kumchafulia umashuhuri wake.

Serkali yagoma kutowa maelezo

Msemaji wa serikali ya Ujerumani alipoulizwa na gazeti la Bild kuhusu repoti hiyo amekaririwa akisema " Serikali ya Ujerumani inaweka imani kubwa kwenye ushirikiano wa kijasusi na Marekani ili kuwalinda raia wetu."

Nembo ya shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA).
Nembo ya shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA).Picha: picture-alliance/dpa

Ameongeza kusema kwamba "serikali haizungumzii kwa kina kuhusu ushirikiano huo hadharani bali jambo hilo hufanywa na kamati za bunge."

Gazeti hilo la Ujerumani limesema limeona nyaraka ambapo kwayo Clapper mkurugenzi wa shirika la usalama wa taifa nchini Marekani alielezea wasi wasi wake kwamba taarifa juu ya ushirikiano huo kutoka ofisi ya kansela kwenda kwa kamati ya bunge zimefichuliwa na kuathiri maslahi ya Marekani.

Kuaminika mashakani

Kwa mujibu wa Bild Clapper amesema Ujerumani haiwezi tena kuaminiwa kwa nyaraka za siri na kadri hali itakavyokuwa hivyo mashirika ya ujasusi ya Marekani yanapaswa kutathmini wapi pa kupunguza ushirikiano wao au kufuta ushirikiano huo na Ujerumani.

James Clapper Mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA).
James Clapper Mkurugenzi wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA).Picha: Reuters

Gazeti hilo la Bild limemkariri afisa huyo wa serikali ya Marekani akisema kuvuja kwa taarifa hizo ni kubaya zaidi kuliko hata taarifa zilizovujishwa na mfanyakazi wa zamani wa NSA Edward Snowden.

Amekaririwa akisema " Kile ambacho serikali ya Ujerumani inachokifanya hivi sasa ni hatari zaidi kuliko hata kile alichokifanya Snowden."

Faragha ni suala nyeti Ujerumani

Wakosoaji wa Merkel wamewashutumu wafanyakazi katika ofisi ya kansela kwa kuruhusu shirika la ujasusi la Ujerumani (BND) kuzipeleleza kampuni za Ulaya na maafisa wake.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/S. Pilick

Uchunguzi wa maoni uliofanyika wiki uliopita umebaini kwamba Mjerumani mmoja katika kila kundi la watu watatu anahisi amedanganywa na Merkel kuhusiana na mzozo wa kuwapeleleza Wajerumani.

Taarifa zilizofichuliwa na Snowden kuhusu ujasusi mkubwa uliofanywa na Marekani nchini Ujerumani ikiwa ni pamoja na madai kwamba mazungumzo ya simu ya mkononi ya Merkel yalikuwa yakitegwa yalichemsha ghadhabu nchini Ujerumani wakati habari hizo zilipoibuka miaka miwili iliopita.

Merkel alisisitiza kwamba BND lazima ishirikiane na NSA kupambana na ugaidi lakini faragha ni suala nyeti nchini Ujerumani baada ya miongo kadhaa ya kupelelezwa na Gestapo na halafu na kikosi cha polisi wa siri cha Stasi kwa iliokuwa Ujerumani Mashariki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ Reuters

Mhariri : Caro Robi