1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutathmini makubaliano kuhusu nyuklia ya Iran

Daniel Gakuba
20 Aprili 2017

Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umesema utayafanyia tathmini mpya makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, uliofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.

https://p.dw.com/p/2bZ8o
USA Iran Gespräche (Symbolbild)
Picha: C. Barria/AFP/Getty Images

Katika mazungumzo na waandishi wa habari, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ameituhumu Iran kufanya kile alichokiita 'uchokozi wa kutisha na unaoendelea' katika kuyumbisha nchi za kanda ya Mashariki ya Kati. Akizungumzia tathmini mpya iliyotangazwa na utawala wa Rais Donald Trump kuhusu Iran, Tillerson amesema Marekani haitayatazama tu makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo, bali pia sera za nchi hiyo katika kanda, ambazo amesema zinahujumu maslahi ya Marekani katika mataifa ya Syria, Iraq, Yemen na Lebanon.

USA Außenminister Rex Tillerson | Vereidigungszeremonie
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex TillersonPicha: Reuters/C. Barria

Maneno yake makali yanafanana na yale yaliyotamkwa na waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis akiwa ziarani nchini Saudi Arabia jana Jumatano, ambapo alisema lazima ushawishi wa Iran uwekewe kikomo, ili kupata amani nchini Yemen.

''Kokote unakotazama katika kanda, kama kuna mzozo, utaikuta Iran. Tunachokishuhudia ni mataifa ya kikanda yanayojaribu kudhibiti kiwango cha kuvuruga utengamani kunakofanywa na Iran'.'' Alisema Mattis, na kuongeza kuwa ''uhusu Yemen, lengo letu ni kushinikiza mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa, katika juhudi za kuumaliza mzozo huu.''

Iran yatimiza majukumu yake kuhusu makubaliano

Pamoja na kauli hizo nzito lakini, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imethibitisha kuwa Iran imeheshimu upande wake wa makubaliano hayo, ambapo ilikubali kupunguza mradi wake wa nguvu za atomiki ili iweze kupunguziwa vikwazo ilivyowekewa na Jumuiya ya Kimataifa.

Katika barua aliyomuandikia Spika wa Baraza la Wawakilishi Paul Ryan, Tillerson amebainisha kuwa Iran imetekeleza majukumu yake kuhusu makubaliano hayo, na kuongeza lakini kuwa upo wasiwasi utokanao na mchango wa Iran katika kile alichokiita ''kufadhili ugaidi''.

Wien Treffen zwischen Kerry und Zarif
Makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yalifikiwa chini ya utawala wa Rais Barack ObamaPicha: Getty Images/AFP/K. Lemarque

Tillerson amesema makubaliano hayo ya mwaka 2015 yanachokifanya ni kuchelewesha tu azma ya Iran kupata silaha za nyuklia, na kusisitiza kuwa utawala wa Trump hautaki kuchelewesha uwajibikaji wa Iran ili ushughulikiwe na serikali zitakazoirithi iliyopo madarakani sasa.

Iran ''kugeuka Korea Kaskazini''

Ameeleza kuwa sera ya Rais Trump kuelekea Iran itajikita juu ya vitisho vyote vya Iran kwa Marekani, akisema isiposhughulikiwa ipasavyo, Iran inaweza kugeuka kitisho kama vile ilivyo Korea Kaskazini.

Msemaji wa Ikulu ya White House mjini Washington Sean Spicer, amesema tathmini mpya kuhusu Iran itashughulikiwa na taasisi za serikali ya Marekani katika kipindi cha siku 90, na kwamba baada ya hapo taasisi hizo zitamshauri Rais Trump ikiwa wanapaswa kuendelea kuyaheshimu makubaliano hayo au la.

Makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yalifikiwa chini ya utawala wa Rais Barack Obama, yakiyahusisha mataifa mengine yenye ushawishi duniani ambayo ni Urusi, Ufaransa, Uingereza, China na Ujerumani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe

Mhariri: Josephat Charo