Marekani kushinikiza kurejeshwa vikwazo dhidi ya Iran
20 Agosti 2020Hatua inayotazamiwa kuongeza kutengwa kwa Marekani katika Umoja huo wa Mataifa na kipimo cha heshima ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia pigo kubwa kwa moja ya mafanikio makubwa ya rais wa zamani Barack Obama kwenye siasa za nje za Marekani.
Kwa muongozo wa Rais Trump, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo atawasili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York leo ili kukifahamisha chombo hicho cha kilimwengu kwamba Marekani inatumia madaraka yake kwenye Baraza la Usalama kuondowa azimio lililoidhinisha Mkataba wa Nyuklia wa Iran mwaka 2015.
Jana Jumatano, Trump alisema kuwa Marekani inadhamiria kutumia kipengele cha utenguzi ili kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilivyokuwa vimesitishwa.
Kipengele hicho ni sehemu ya kanuni za Baraza la Usalama, ambazo pia zinatowa uhalali kwa taifa lolote kuchukuliwa hatua endapo haliheshimu maamuzi ya utenguzi wa azimio siku 30 tangu utenguzi ufanyike.
Upinzani mkali kutoka kwa mataifa mengine
Hata hivyo, uamuzi huu wa Marekani unakabiliwa na upinzani mkali na unaweza kuchochea aina fulani ya uasi kutoka wajumbe wa Baraza la Usalama, kwani hakuna hata mmoja miongoni mwao anayeamini kuwa Marekani ina hoja ya kusimamia kwenye hili, kwa kuwa mwenyewe Trump alishaiondowa nchi yake kwenye mkataba huo tangu miaka miwili iliyopita.
Tayari, Urusi imeuelezea uamuzi huo kuwa wa kipuuzi, ikisema kwamba hauna mashiko ya kisheria wala kisiasa.
Shirika la habari la nchi hiyo, RIA, limemnukuu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Ryabkov hivi leo akisema kwamba kitu pekee ambacho Marekani itafanikiwa kwenye uamuzi wake huu ni kuchochea mzozo ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Pompeo awatunishia misuli wapinzani wa Marekani
Pompeo amezionya Urusi na China, zote wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, kutokuudharau uamuzi wa Marekani kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa kwa Iran, lakini ni wazi kuwa tayari mataifa hayo yameshaudharau.
Ikiwa Marekani itaendelea na uamuzi wake wa kurejesha vikwazo hivyo bila ridhaa ya Baraza la Usalama, heshima ya Baraza hilo itakuwa mashakani, kwani itaonesha jinsi lisivyo na nguvu za kisheria kulazimisha maamuzi yake kutekelezwa.
Lakini Trump na Pompeo hawafanyi siri kwamba dhamira yao ni kuchukuwa hatua hiyo yenye utata hasa baada ya wiki iliyopita kushindwa kwenye Baraza hilo hilo kuongeza muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran unaomalizika mwezi Oktoba mwaka huu. Kwenye kikao hicho, Marekani ilipata kura moja tu ya ndio, huku China na Urusi zikipinga na wajumbe wengine 11 wakijizuwia kupiga kura zao.
Kama ilivyokuwa kwa suala la vikwazo vya silaha, Urusi na China zinapingana pia na kurejeshwa vikwazo vyengine vya Umoja wa Mataifa kwa Iran, msimamo unaoungwa mkono pia na wanachama wengine wa Baraza la Usalama, wakiwemo washirika wakubwa wa Marekani, yaani Ufaransa na Uingereza.
Wote wanataka kuendelea kusalia na Mkataba wa Nyuklia na Iran uliosainiwa mwaka 2015, huku wakitazamia endapo utawala wa Marekani utabadilika kwenye uchaguzi wa Novemba mwaka huu na Joe Biden kuingia madarakani, watashirikiana kuhakikisha utekelezwaji wa vipengele vilivyobakia.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri:Iddi Ssessanga