1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuondoa wanajeshi wake Afghanistan

24 Juni 2011

Rais Barack Obama wa Marekani jana aliamuru wanajeshi wote 33,000 waliopelekwa nchini Afghanistan kwa ziada warejee nyumbani ifikapo majira ya joto mwakani.

https://p.dw.com/p/11i4i
Wanajeshi wa Marekani wakiwa Helmand, AfghanistanPicha: picture alliance/dpa

Kiongozi huyo pia ametangaza mwanzo wa kumalizika kwa vita , na kuahidi kugeukia hatua za ujenzi wa taifa nchini Marekani.

Katika wakati wa mabadiliko makubwa ya sera za mambo ya kigeni ya Marekani, Obama pia kwa kiasi kikubwa amepunguza malengo ya kivita ya Marekani , akisema kuwa nchi hiyo haiwezi tena kujaribu kuijenga Afghanistan sahihi kutoka taifa hilo lililokumbwa na matatizo kutokana na historia yake ya umwagaji wa damu.

Obama während der Rede an die Nation
Rais Barack Obama akitoa hotuba Whitehouse: Wanajeshi kuondoka Afghanistan mwakaniPicha: AP

Changamoto na majukumu

Leo tunajisikia wenye afueni kwa kutambua kuwa wimbi la vita linapungua, Obama amesema katika hotuba yake ya dakika 13, katika wakati ambapo kuna ongezeko la uchovu kuhusiana na gharama za vita nchi za nje miongoni mwa Wamarekani ambao wanakabiliwa na hali ngumu isiyojulikana ya kiuchumi.

Hata iwapo kutakuwa na nyakati ngumu mbele nchini Afghanistan, mwanga wa kupatikana amani unaweza kuonekana kwa mbali. Vita hivi virefu vitafikia mwisho hatimaye: " Ni dhahiri kwamba changamoto kubwa bado zipo. Huu ni mwanzo, sio mwisho wa juhudi zetu za kufikisha mwisho vita hivi. Tunapaswa kufanya kazi ngumu ya kuendeleza mafanikio tuliyoyapata," amesema Obama.

Taliban na mapambano

Rais Obama amedai kuwa majeshi ya Marekani yamepata mafanikio makubwa kuelekea katika malengo ya mkakati wa kupeleka wanajeshi wa ziada , alioamuru Desemba 2009 kwa kurejesha nyuma juhudi za Taliban, kuipa kipigo al-Qaeda na kulipa mafunzo jeshi jipya la Afghanistan. Lakini amekataa miito ya wizara ya ulinzi ya kufanya upunguzaji huo kwa taratibu ili kulinda mafanikio dhidi ya Taliban na uamuzi wake utaonekana kuwa ni kushindwa kisiasa kwa jenerali mwenye sifa ya kutoa dawa ya mzozo huo David Petraeus. Barack Obama amesema: " Wakati tukipunguza majeshi yetu tunakabidhi majukumu ya mpito kwa ajili ya usalama wa ndani kwa majeshi ya Afghanistan. May mwakani mjini Chicago , tutafanya mkutano pamoja na washirika wetu wa NATO na washirika wengine, kuangalia jinsi ya kupanga utaratibu mwingine wa mpito."

Friedens-Dschirga in Kabul Afghanistan Hamid Karzai Flash-Galerie
Rais Hamid Karzai akitoa hotuba kwenye kikao cha baraza la Usalama Afghanistan: Jirga.Picha: AP

Atimiza ahadi

Rais amesema kuwa , kama alivyoahidi, kwamba atayaondoa majeshi ya Marekani kutoka Afghanistan kuanzia Julai na kwamba wanajeshi 10,000 miongoni mwa zaidi ya wanajeshi 30,000 aliowapeleka watarejea nyumbani mwaka huu.

Hata hivyo licha ya maneno ya kutia moyo ya rais Obama , inawezekana wapiganaji wa Taliban wakapata nguvu kutokana na ishara za kuharakishwa kuondoka majeshi ya Marekani kutoka katika mzozo huo. Zaidi ya wanajeshi 1,600 wa Marekani wameuwawa nchini Afghanistan tangu uvamizi wa Marekani baada ya shambulio la Septemba 11, 2001.

Taliban in Kandahar Afghanistan
Wapiganaji wa Taleban wakijisalimisha KandaharPicha: picture-alliance/Photoshot

Vifo vya wanajeshi wa Marekani kwa mwaka huu vimefikia hadi sasa wanajeshi 187.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre

Mhariri: Abdu Mtullya