1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Marekani kufanya hivyo

8 Aprili 2019

Marekani inapanga kuliorodhesha jeshi la Mapinduzi ya Iran kuwa miongoni mwa makundi ya kigaidi.

https://p.dw.com/p/3GSiS
Iran Revolutionsgarden
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Noroozi

Maafisa wawili wa serikali ya Marekani na bunge walithibitisha hilo japokuwa hawaruhusiwi kulizungumza suala hilo hadharani, hivyo waliyasema hayo kwa misingi ya kutotaka majina yao kujulikana.

Hatua hiyo ya Marekani ambayo mwanzo iliripotiwa na gazeti la Marekani la Wall Street inapanga pia kuweka vikwazo mbalimbali ikiwemo kutaifisha mali ya jeshi hilo zilizoko Marekani na kupiga marufuku Wamarekani kufanya biashara na jeshi hilo ama kulisaidia kwa njia yoyote ile.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Marekani kukiorodhesha kikosi cha jeshi la nchi nyingine kuwa miongoni mwa makundi ya kigaidi ijapokuwa serikali zilizopita za Marekani zilikuwa zimekilenga kikosi kingine cha Iran cha Quds kukiweka miongoni mwa makundi ya kigaidi.

München MSC Javed Zarif
Waziri wa masuala ya kigeni wa Ira, Javad ZarifPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Joensson

Waziri wa masuala ya kigeni wa Iran, Javad Zarif katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Twitter akimlenga Rais wa Marekani, Donald Trump akisema anapaswa kufahamu kwa kina kuliko kuitumbukiza Marekani katika janga jengine.

Jeshi la Mapinduzi ya Iran lina udhibiti mkubwa na ushawishi katika uchumi wa Iran hivyo vikwazo vya Marekani dhidi yake havina athari kubwa na badala yake vitatatiza pakubwa masuala kijeshi na ya kidiplomasia ya serikali ya Marekani hasa nchini Iraq ambako makundi mengi ya wanamgambo wa Kishia na vyama vya kisiasa vya Iraq vina uhusiano wa karibu na kikosi hicho.

Zaidi nchini Lebanon itakuwa Marekani imejiongezea vizuizi yenyewe na kushindwa kujua afisa yupi wa kushirikiana naye kwa sababu jeshi hilo lina mafungamano na Hezbollah kundi ambalo ni sehemu ya serikali ya Lebanon. Tayari Marekani inalitambua kundi la Hezbollah kuwa kundi la kigaidi na uwepo wake katika bunge na baraza la mawaziri la Lebanon imeilazimisha Marekani kuiepuka serikali ya Lebanon japokuwa inaendelea kulisaidia na kufanya kazi na jeshi la Lebanon.

Iranische Revolutionsgarde
Wanajeshi wa jeshi la Mapinduzi ya Iran.Picha: AP

Taasisi mbali mbali za Marekanii hazipokea vyema wazo hilo.

Wizara ya ulinzi na taasisi za ujasusi nchini Marekani zilionyesha wasiwasi wao juu ya athari ya uamuzi huo iwapo hatua hiyo haitaruhusu kuwasiliana na maafisa wa kigeni ambao wamewahi kushirikiana ama kuwasiliana na wakuu wa vikosi hivyo vya mapinduzi. Wasiwasi huo ndio kwa kiasi ulizuia serikali zilizopita za Marekani kuchukua uamuzi ambao umekuwa ukifikiriwa kwa miongo kadhaa.

Afisa mwengine wa serikali ya Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa alisema makamanda wa jeshi la Marekani pia wameingia wasiwasi kwa hatua hiyo akisema inaweza kuifanya Iran nayo kulipiza kwa kuviwekea vikwazo vikosi vya majeshi ya Marekani ambavyo vimebakia Iraq, Syria, na kwengineko katika kanda hiyo na kwamba makamanda hao wanapanga kuitahadharisha Marekani juu ya hilo.

Syrien US Soldaten bei Manbidsch
Wanajeshi wa Marekanni wakiwa nchini SyriaPicha: picture-alliance/AP/U.S. Army/Spc. Z. Garbarino

Vile vile onyo jengine lilitarajiwa kutoka katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu uwezekano wa Iran kulipiza kisasi dhidi ya maslahi ya Marekani ikiwemo ubalozi na ofisi ndogo za ubalozi na maandamano ya kuipinga serikali ya Marekani. Tahadhari kama hizo ziliwahi kutolewa mwanzoni mwa vita vya Iraq mwaka 2003 na hivi karibuni baada ya Rais Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Mbali na wanajeshi wa Marekani 5,200 walioko nchini Iraq, nchini Syria Marekani ina wanajeshi 200 na kikosi chengine kinachofanya operesheni zake katika Ghuba ya Kiajemi kambi yake ikiwa Bahrain na Qatar zote ziko katika hatari ya kuathiriwa na uamuzi huo wa Marekani ambao iwapo bunge la Marekani litaupitisha basi utatekelezwa mara moja.

(APE)