1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuliandama kundi la ISIL

21 Agosti 2014

Marekani imefanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu lililomchinja mwandishi wa habari wa Marekani James Foley na ambalo limeteka sehemu kubwa ya ardhi nchini Iraq na Syria.

https://p.dw.com/p/1Cycx
Wapiganaji wa ISIL katika mpaka kati ya Syria na Iraq.
Wapiganaji wa ISIL katika mpaka kati ya Syria na Iraq.Picha: picture-alliance/dpa

Dunia imefadhaishwa na kitendo cha kuchinjwa kwa mwandishi huyo ambapo shirika la polisi la kimataifa Interpol limetowa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za pamoja za kimataifa kupambana na waasi hao. Mohamed Dahman na taarifa kamili.

Rais Barack Obama wa Marekani ameapa kwamba atawaandama hadi mwisho magaidi hao wakati Ikulu ya Marekani ikisema ilifanya operesheni ya siri kumuokowa mwandishi huyo na mateka wengine wanaoshikiliwa nchini Syria mapema katika kipindi hiki cha kiangazi ambayo imeshindwa.

Operesheni hiyo ya siri ya kuwaokowa mateka wa Marekani ilivihusisha vikosi kadhaa maalum vilivyodondoshwa nchini Syria kwa ndege.Mateka hao hawakuweza kupatikana lakini vikosi hivyo vilishambuliana kwa risasi na wanamgambo wa Dola la Kiislamu kabla ya kuondoka, wanamgambo kadhaa waliuwawa na mwanajeshi mmoja wa Marekani alijeruhiwa.

Katika matamshi mafupi lakini makali Rais Obama hapo jana amesema Marekani itafanya kila inacholazimika kufanya kuwalinda watu wake lakini amesita kuahidi kuwaandama wanamgambo wa kundi la Dola la Kiilamu hadi kwenye maficho yao nchini Syria ambapo serikali inasema ndiko alikouwawa mwandishi huyo.

ISIL ni muflisi wa itikadi

Obama amekaririwa akisema "ISIL haisimamii dini yoyote. Wahanga wao wengi ni Waislamu na hakuna dini inayofunza watu kuchinja watu wasiokuwa na hatia.Hakuna mungu wa haki atakayetetea kile walichokifanya jana na kile wanachofanya kila siku.ISIL haina itikadi yenye kuthamini binaadamu.Itikadi yao imefilisika"

Rais Barack Obama akitowa taarifa kufuatia kuuwawa kwa mwandishi James Foley. (20,08.2014)
Rais Barack Obama akitowa taarifa kufuatia kuuwawa kwa mwandishi James Foley. (20,08.2014)Picha: Reuters

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani haikufuta uwezekano wa kufanya operesheni za kijeshi huko usoni nchini Syria ambapo Obama kwa muda mrefu amekuwa akikataa kuingilia kati katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitatu.

Shirika la polisi la kimataifa Interpol limesema katika taarifa leo hii kwamba kifo cha mwandishi James Foley kinaonyesha upotovu wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria na Iraq na kubainisha hali inayoendelea kuwakabili watu wengine wasiokuwa na hatia katika eneo hilo.

Wapiganaji wa kigeni

Shirika hilo lenye makao yake nchini Ufaransa limezidi kuwa na wasi wasi kutokana na mtu alionekana kwenye mkanda wa video ya kifo cha Fowley kuwa na lafidhi ya Kingereza jambo ambalo limeonyesha haja ya kuchukuliwa kwa hatua ya pamoja ya kimataifa dhidi ya tishio hilo la kigaidi linatokana na wapiganaji wa kimataifa wanaosafiri kwenda kwenye maeneo ya mizozo huko Mashariki ya Kati.

Omar al-Shishani kutoka Chechnya miongoni mwa mamia ya wapiganaji wa kigeni walioko katika kundi la ISIL.
Omar al-Shishani kutoka Chechnya miongoni mwa mamia ya wapiganaji wa kigeni walioko katika kundi la ISIL.Picha: picture alliance/AP Photo

Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott na Rais Susilo Bambang Yodhoyono wa Indonesia wamelaani kitendo cha kuchinjwa kwa mwandishi huyo wa Marekani na kuonya juu ya kundi hilo la Dola la Kiislamu.

Wakati Yudhoyono akisema kuwa ni kitendo cha kufadhaisha na kwamba kundi hilo halidhibitiki tena Abbot amesema ataendeleza ushirikiano wa karibu wa usalama na Indonesia ambapo kundi la Jemaah Islamiya lilioko Indonesia na lililohusika na miripuko ya mabomu ya Bali mwaka 2002 limeelezea kuunga mkono kwake kundi hilo la Dola la Kiislamu.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri: Josephat Charo