1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama atangaza kuendeleza vita dhidi ya IS

7 Julai 2015

Rais wa Marekani Barack Obama amesema jeshi la muungano linaloongozwa na Marekani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu - IS "litaimarisha" kampeni yake katika ngome muhimu ya kundi hilo nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1FtoK
Obama - Terrorbekämpfung
Picha: Reuters

Obama alizungumza na vyombo vya habari baada ya kufanya mkutano na maafisa wakuu wa jeshi pamoja na kikosi chake cha usalama wa taifa katika wizra ya ulinzi Pentagon kuhusu juhudi za kulisambaratisha kundi hilo la jihadi, ambalo limeyakamata maeneo makubwa ya Iraq na Syria. "Mashambulizi yetu yataendelea kuvilenga vituo vya mafuta na gesi ambavyo hutumiwa kugharamia operesheni zao. Tutaulenga uongozi wa IS na miundo mbinu nchini Syria, kitovu cha IS ambacho hutoa fedha na propaganda kwa watu kote ulimwenguni".

Luftangriffe auf Zabadani Syrien ARCHIV
Mji wa Zabadini umekumbwa na mapigano makaliPicha: picture alliance/abaca

Mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yalikuja baada ya mashambulizi ya kutokea angani kuulenga mji wa Raqqa mwishoni mwa wiki – ikiwa ni mojawapo ya mashambulizi makali zaidi kuwahi kufanywa tangu muungano huo ulipoanza kupambana na IS nchini Syria mwezi Septemba. Obama hata hivyo alionya kuwa vita dhidi ya kundi hilo la itikadi kali vinaweza kukabiliwa na changamoto. "Hii ni kampeni ya muda mrefu. IS ni kundi mahiri ambalo katika maeneo mengi ya Syria na Iraq, yakiwemo maeneo ya mijini, limejificha kabisa miongoni mwa raia wasio na hatia. itachukua muda kuwang'oa. na kutimiza hilo lazima iwe kazi ya majeshi yalioko huko, kwa kupewa mafunzo na msaada wa angani kutoka kwa muungano wetu".

Alisema zaidi ya mashambulizi 5,000 ya kutokea angani yamefanywa dhidi ya kundi hilo, na kuwaangamiza “maelfu ya wapiganaji”, wakiwemo makamanda wakuu wa IS. Rais wa Marekani amesema mengi yanahitaji kufanywa ili kuwafunza wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa Kisunni nchini Iraq, pamoja na waasi wa misimamo ya wastani nchini Syria.

Hapo awali, Waziri wa Ulinzi Ashton Carter alisema mashambulizi hayo ya mwishoni mwa wiki hayakuwalenga wapiganaji Fulani wa IS, lakini yalikuwa sehemu ya juhudi za kuwasaidia wanajeshi wa Kikurdi na “kupunguza uhuru wa IS kuendesha harakati zake”.

Shirika linalofuatilia matukio ya ukiukaji wa haki za binaadamu la Syria limesema mashambulizi hayo yaliwauwa karibu watu 30, miongoni mwao raia sita akiwemo mtoto mmoja.

Waziri Carter anatarajiwa kufika leo mbele ya Kamati ya Baraza la Seneti kuhusu masuala ya ulinzi ili kuijadili kampeni hiyo, ambayo imekosolewa upya na wabunge wa Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir