Marekani kuendelea na mashambulizi Iraq
22 Agosti 2014Akizungumza na waandishi wa habari, waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel kwanza alielezea kusikitishwa kwake na kifo cha kinyama cha mwandishi wa habari James Foley. Wanamgambo wa Dola la Kiislamu hivi karibuni waliweka video mtandaoni inayoonyesha Foley akikatwa shingo. "Marekani ilijaribu kuwakomboa baadhi ya mateka waliokuwa wakishikiliwa Syria, mmoja wao akiwa James Foley.," alisema Hagel. "Tunasikitika kwamba operesheni hiyo haikuwa na mafanikio lakini tunajivunia wanajesi wa Marekani walioshirikia katika juhudi za kukomboa mateka."
Hagel aliongezea kwamba Marekani haitapunguza juhudi za kuwarudisha mateka nyumbani na vile vile kuhakikisha kuwa waliowateka nyara wanapelekwa mbele ya sheria. Kinachowaumiza Wamarekani kichwa ni kwamba wanamgambo wa Dola la Kiislamu wanaonekana kuwa na wafadhili wengi wanaowapa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununua silaha.
Gazeti la Global Post lililokuwa limemwajiri Foley, linaeleza kwamba Dola la Kiislamu lilitaka Marekani itoe dola milioni 130 kama malipo ya kumwachia huru Foley. Lakini Marekani ilikataa kufanya hivyo, ikisema kwamba haitajadiliana na magaidi.
Silaha zaanza kuwasili kwa Wakurdi
Viongozi wa Dola la Kiislamu wameapa kumuuwa mwandishi wa habari mwingine iwapo Marekani haitasimamisha mashambulizi ya anga katika eneo la Iraq ya Kaskazini. Lakini tamko hilo halielekei kuitishia Marekani kwani nchi hiyo imesema itaendeleza mashambulizi.
Wakati huo huo, nchi kadhaa za Magharibi ikiwemo Ujerumani, zimeanza kuwasilisha silaha kwa wapiganaji wa Kikurdi ili waweze kuwakabili waasi wa Dola la Kiislamu.
Mmoja wa majenerali ameeleza kwamba Wakurdi hawahitaji nchi nyingine zitume wanajeshi, wanachohitaji ni silaha. "Najua kuwa silaha mpya zimewasili lakini tunahitaji kufundishwa namna ya kuzitumia. Kwa sasa tuna silaha zetu za zamani tu. Nimesikia kuwa baadhi ya Wakurdi wameanza kupewa mafunzo na silaha, sisi bado. Lakini naamini kuwa inshallah tutazipata hivi karibuni," alisema jenerali huyo.
Alisisitiza pia kwamba anataka ulimwengu ufahamu kuwa Wakurdi wanapigana kwa niaba ya jumuiya ya kimataifa na si kwa manufaa yao binafsi.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/ap
Mhariri: Saumu Yusuf