Marekani kuchukua hatua dhidi ya Urusi kufuatia udukuzi
16 Desemba 2016Marekani itachukua hatua dhidi ya Urusi kufuatia madai ya nchi hiyo kudukua masuala ya uchaguzi ya Marekani. Hayo yamesemwa na Rais Barrack Obama alipohojiwa na runinga ya NPR. Wakati huo huo, Rais Mteule Donald Trump amesema atamteua David Friedman kuwa balozi wa Marekani nchini Israel.
Maafisa wa shirika la ujasusi la Marekani, CIA wamesema wanayo imani ya hali ya juu kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin alihusika kuamuru jinsi taarifa ambazo wadukuzi walipata zilifichuliwa. Runinga ya ABC imetangaza.
Wadukuzi wa Urusi walidukua barua pepe za Kamati Kuu na za maafisa wakuu wa chama cha Democrat zikiwemo za aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni ya Hillary Clinton, John Podesta.
Barua pepe hizo zilichapishwa mwezi mmoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Urais Marekani, hali ambayo majasusi wa CIA walisema ilinuia kushawishi uchaguzi huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa shirika la CIA limefikia kuwa lengo la Urusi lilikuwa ni kumsaidia Trump kutwaa ushindi. Obama hakulaumu hayo kuchangia kushindwa kwa Hillary Clinton lakini amekosoa Urusi kuingilia masuala ya uchaguzi wa Marekani. Hii hapa kauli ya Obama alipohojiwa na runinga ya NPR.
''Ninafikiri hakuna tashwishi kwamba nchi ya nje inapoingilia uadilifu wa uchaguzi wetu, tunapaswa kuchukua hatua, na bila shaka tutachukua hatua wakati tutakaochagua sisi wenyewe. Baadhi ya hatua hizo zinaweza kuwa dhahiri na kuchapishwa nyingine sivyo. Bwana Putin anafahamu hisia zangu kuhusu suala hili kwa sababu niliongea naye moja kwa moja kulihusu.''
Hata hivyo washirika wa Putin na hata Rais Mteule Donald Trump wamepuuzia madai kuwa udukuzi huo ulikuwa na malengo maalum.
Kuhusu uundaji wa serikali yake, Donald Trump ametangaza kuwa atamteua David Friedman kuiwakilisha Marekani nchini Israel kama balozi.
Friedman anayeunga mkono ujenzi wa makaazi Israel na mabadiliko mengine katika sera za Marekani kuhusu Mashariki ya Kati amesema ananuia kutekeleza majukumu yake katika jiji kuu la ndani ya Israel, Yerusalem, japo ubalozi upo katika jiji la Tel Aviv.
Kama ilivyokuwa kwa baadhi ya watangulizi wake, Trump anataka kuuhamisha ubalozi wa Marekani hadi Yerusalem, hatua ya kisiasa itakayowakasirisha Wapalestina ambao wanataka mashariki ya Yerusalem kuwa sehemu ya nchi yao.
Trump amesema Friedman ataendeleza uhusiano wa kipekee kati ya Marekani na Israel. Lakini tangazo hilo limeibua shutuma kutoka kwa makundi ya kiliberali ya kiyahudi. Jeremy Ben- Ami ambaye ni mkuu wa J Street amesema uteuzi wa Friedman ni ukosefu wa uangalifu wa makini. Amerejelea uungwaji mkono wa Friedman wa makaazi ya Israel.
Mwandishi: John Juma/DPE/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo