1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuchukua hatua dhidi ya Korea Kaskazini

Yusra Buwayhid
3 Aprili 2017

Rais Donald Trump amesema Marekeni imejitayarisha yenyewe, kuchukua hatua dhidi ya mpango wa kinyuklia wa Korea Kaskazini iwapo China haitokuwa na msimamo madhubuti.

https://p.dw.com/p/2aXbE
U.S. Präsident Donald Trump Republican Congressional Committee Rede
Picha: Reuters/C. Barria

Matamshi hayo ya Trump katika mahojiano na Gazeti la biashara la kimataifa la Financial Times la Uingereza, yamekuja siku chache kabla ya kiongozi huyo kukutana na Rais wa China Xi Jinping katika jimbo la Florida baadaye wiki hii. 

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na Korea Kaskazini, mahusiano ya kibiashara na mizozo ya mipaka katika Bahari ya Kusini ya China wakati wa mkutano wao utakaofanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa.

Akizungumza na gazeti hilo, Trump amekiri kuwa mazungumzo hayo yatajumuisha pia suala la Korea Kaskazini. Trump ameongeza kuwa China ina ushawishi mkubwa juu ya Korea Kaskazini.

"China ama itaamua kuisaidia Marekani katika suala la Korea Kaskazini, au itakataa. Na iwapo China itaamua kutoa msaada wake basi hilo litakuwa jambo zuri kwa China, kinyume na hilo, halitokuwa jambo zuri kwa mtu yoyote," amesema Donald Trump.

Trump alipoulizwa Marekani itatumia motisha gani kuishawishi China, alisema kuwa ni biashara.

Msemaji mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema Waziri wa Mambo ya nje Rex Tillerson, amekuwa na mawasiliano na maafisa wa ngazi za juu wa China kuhusu mkutano huo.

Uhusiano wa Marekani na China ni wa wasiwasi

Bildkombo Xi Jinping und Donald Trump
Rais wa China Xi Jinping (kushoto) na Rais wa Marekani Donald Trump (kulia)Picha: Reuters/T. Melville/M. Segar

Uhusiano kati ya Marekani na China, umekuwa wa wasiwasi tangu Trump alipoingia madarakani.

Wakati wa kampeni zake za uchaguzi, Trump ameishutumu China kwa kufanya biashara isiyo ya haki, alitishia kupandisha kodi ya bidhaa za Kichina zinazoingizwa nchini Marekani, na pia alisema China inaitumia vibaya sarafu yake.

Hata hivyo haijulikani kama Trump atachukuwa hatua zozote kuhusu vitisho hivyo dhidi ya China.

Haijulikani ni njia gani ambazo Marekani itatumia kuizuia Korea Kaskani kuimarisha uwezo wake wa kinyuklia, kuendeleza uundaji wa makombora ya masafa marefu, na uwezo wa kutengeneza vichwa vya nyuklia.

Umoja wa Mataifa umeshindwa suala la Korea Kaskazini

Umoja wa Mataifa hadi sasa umeshindwa kuizuia Korea Kaskazini kuendesha majaribio yake ya kinyuklia na ya makombora. Mwaka jana, Korea Kaskazini ilifanya majaribio mawili ya kinyuklia na majaribio mengine kadhaa ya makombora ya masafa marefu.

Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa, Nikki Haley, amesema China lazima iishinikize Korea Kaskazini. Ameongeza kuwa nchi pekee inayoweza kuizuia Korea Kaskazini ni China, na hilo wanalijua.

Trump na Xi pia wanatarajiwa kujadili azma ya China katika Bahari ya Kusini ya China, njia ambayo meli za biashara yenye thamani ya karibu trilioni 5 zinapita kila mwaka. China inadai umiliki wa eneo kubwa la Bahari ya Kusini ya China yenye wingi wa rasilmali, huku Brunei, Malaysia, Ufilipino, Taiwan na Vietnam pia zikidai umiliki wa njia hiyo ya kimkakati.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri: Josephat Charo