Marekani kuanza kutoa upya misaada kwa Palestina
27 Januari 2021Utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden umetangaza kurejesha uhusiano na Palestina na kuanza kutoa upya misaada kwa wakimbizi wa Palestina. Hiyo ni hatua inayoonyesha sera ya Biden ya kutaka kuweko na mataifa mawili kufuatia mzozo wa miongo kadhaa baina ya Israel na Palestina.
Taarifa hiyo ilitolewa na kaimu balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Richard Mills wakati wa kikao kwa njia ya video cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mills amesema utawala wa Biden umehisi kwamba kuweko na mataifa mawili ni njia muafaka kwa ujio wa Waisraeli na Wapalestina.
'' Chini ya utawala mpya, sera ya Marekani itakuwa ni kuunga mkono suluhisho la kuwepo na mataifa mawili, ambamo Israel inaishi kwa amani na usalama sambamba na taifa la Wapalestina. Mtazamo huo ingawa unakabiliwa na changamoto ,unabaki kuwa njia bora zaidi ya kuhakikisha mustakabali wa Israel kama taifa la kidemokrasia na la Kiyahudi, huku tukiunga mkono madhumuni ya Wapalestina ya kuishi katika taifa lao kwa heshima na usalama''
Biden na sera mpya ya Mashariki ya Kati
Utawala wa rais Donald Trump ulitoa ungwaji mkono mkubwa kwa Israel, kwa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuhamishia ubalozi wake kutoka Tel Aviv, kupunguza misaada kwa Wapalestina na kutojali ujenzi wa makaazi ya waloezi kwenye ardhi inayodaiwa ya Wapalestina.
Israel ilidhibiti Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Maragharibi wakati wa vita vya mwaka 1967. Jumuiya ya Kimataifa imeyatambua maeneo hayo yote mawili kuwa maeneo yanayokaliwa, na Wapalestina wanayadai kuwa ardhi yao katika taifa huru litakaloundwa. Toka wakati huo Israel ilijenga makaazi zaidi ya laki saba ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki.
Mpango wa amani uliotangazwa na Trump mwaka mmoja uliopita ulilenga kuweko na taifa la Palestina ambalo limeiachia Israel maeneo muhimu ya Ukingo wa Magharibi.
''Amani haiwezi kulazimishwa''
Mpango huo uliinyemelea pia Israel katika masuala muhimu yanayozozaniwa yakiwemo mipaka, ardhi ya Jerusalem na ujenzi wa makaazi ya Waloezi. Mpango huo wa amani wa Trump ulitupiliwa mbali na Wapalestina.
Richard Mills aliweka wazi mtazamo wa utawala wa Biden kuhusu mpango usionyemelea upande wowote wa mzozo baina ya Israel na Palestina.
Mills amesema kwamba amani haiwezi kulazimishwa kwa upande wowote ule, na kusisitiza kwamba maendeleo na suluhisho la kudumu litatokana na mchango na ridhaa ya Waisrael na Wapalestina.