Marekani, Kenya zatazamia kuimarisha uhusiano wa kibiashara
25 Mei 2024Marekani na Kenya zimesema jana kuwa zitafanya duru mpya ya mazungumzo ya biashara mwezi ujao, wakati mataifa hayo mawili yakipigia debe makubaliano mapya ya biashara na yakitazamia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
Rais wa Kenya William Ruto alikuwa mjini Washington kwa ziara ya kitaifa wakati Ikulu ya White House ilipoahidi ushirikiano mpya kuhusu teknolojia, usalama na msamaha wa madeni kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.
Soma pia: Biden, Ruto waahidi kulinda demokrasia Afrika na kwingineko
Rais Ruto aliahidi kurahisisha ufanyaji biashara nchini Kenya wakati akiwavutia wafanyabiashara kuwekeza nchini mwake.
Waziri wa biashara wa Marekani Gina Raimondo aliwahimiza viongozi wa biashara kuendeleza kasi baada ya matukio ya wiki hii, na kuwataka waingie makubaliano kuwekeza Kenya na Afrika kwa ujumla.
Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani ilisema mataifa hayo mawili yatafanya duru ya sita ya majadiliano mjini Mombasa kuanzia Juni 3 hadi 7 baada ya mazungumzo ya mjini Washinton mwezi huu.