Marekani izungumza na Korea Kaskazini
6 Machi 2007Kabla ya mkutano huo, pande zote mbili zimejitahidi kuonyesha kuwa ziko tayari kuafikiana. Ijumaa iliyopita, Korea Kaskazini imethibitisha kuwa inataka kusimamisha kituo chake cha kinyuklia na kuweka wazi miradi yake ya kinyuklia. Marekani pia inaonekana inabadilisha msimamo wake. Kwanza, imekubali kufanya mkutano wa ana kwa ana ambao hadi sasa imeukataa. Pili, serikali ya Washington, wiki iliyopita, iliarifu kuwa itapunguza vikwazo vya kifedha dhidi ya Korea Kaskazini. Vikwazo hivi vinahusu hasa kiasi cha Dola millioni 24 za Kimarekani ambazo zimewekwa kwenye akauti 40 katika Benki ya Delta Asia huko Makao, Uchina, fedha ambazo tangu mwaka mmoja na unusu sasa zimezuiliwa.
Marekani inaituhumu Korea Kaskazini kwa kutumia akaunti hizo kufanya biashara ya magendo. Inasemekana kuwa nusu ya fedha hizo zitapatikana tena.
Jambo la tatu ni kuwa kwa mara ya kwanza serikali ya rais Bush imetaja mashaka ikiwa kweli Korea Kaskazini ina mradi mwingine wa kinyuklia na hivyo kudhoofisha sababu za mzozo huu wa sasa. Alipoongea mbele ya bunge, afisa moja wa cheo cha juu katika idara za ujasusi ya Marekani alisema hakuna uhakika tena iwapo Korea Kaskazini, pamoja na kutengeneza Plutonium pia inatengeneza Uranium ambayo inaweza kutumika kutengeneza mabomu ya kinyuklia.
Mzozo huu umeanzishwa mnamo mwaka 2002 baada ya Marekani kuilaani Korea Kaskazini kwa kurutubisha madini ya Uranium kisirisiri. Sasa lakini mpatanishi mkuu wa Marekani katika suala hilo na Korea Kaskazini alisema kuna mashaka Korea Kaskazini imefika wapi katika utaratibu huu wa kurutubisha Uranium.
Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia. IAEO, Mohammed El Baradei alipongeza mkutano huu kati ya Marekani na Korea Kaskazini kufanyika. Aslisema: “Hii ni mara ya kwanza ambapo tunaona hatua kamili ya kubadilisha mwenendo na kushirikiana kama jumuiya ya kimataifa katika kufuta kabisa miradi ya kinyuklia kwenye eneo la Korea na kukaribia maafikiano.”
Katika uchambuzi uliochapishwa katika gazeti la New York Times, mhariri huyu ameandika kuwa Marekani imetumia ukweli kulingana na matumizi yake, yaani ukosefu wa uhakika juu ya mradi wa kurutubisha Uranium uliwekwa wazi tu baada ya Korea Kaskazini kuwakubali maafisa wa IAEO kuingia nchi hiyo.