Marekani haipingi mfumo wa biashara wa Ulaya kuisaidia Iran
31 Mei 2019Iwapo tu lengo ni kutoa huduma ya kiutu na bidhaa nyingine zilizoruhusiwa hilo halina taabu. Pompeo ameyasema hayo mbele ya waandishi habari baada ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas.
Pompeo akifanya ziara yake ya kwanza nchini Ujerumani akiwa waziri wa mambo ya kigeni , amesema Marekani haizuwii utayarishaji wa mfumo unaofahamika kama INSTEX, iwapo tu utashughulika na biashara ya bidhaa ambazo hazimo katika orodha iliyowekewa vikwazo, kama ambavyo mataifa ya Ulaya yanavyofikiria kuwa itakuwa hivyo.
"tumekuwa wawazi kabisa juu ya biashara na Iran, kuna bidhaa ambazo zimewekewa vikwazo na kuna bidhaa ambazo hazikuwekewa vikwazo," Pompeo amewaambia waandishi habari baada ya mkutano na waziri mwenzanke wa Ujerumani Heiko Maas katika jengo la serikali mjini Berlin.
"Wakati tukifikiri kuhusu INSTEX , iwapo mfumo huu unalenga katika kutoa huduma ya usafirishaji wa bidhaa ambazo zinaruhusiwa kusafirishwa, hakuna taabu," alisema. Pompeo alikutana kwanza na kansela Angela Merkel wa Ujerumani kabla ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas.
Jinsi ya kuizuwia Iran
Pompeo aliwaambia waandishi habari kabla ya kuanza ziara yake nchini Ujerumani kwamba mazungumzo yatatuwama katika makubaliano ya kinyuklia na Iran, masuala yanayolihusu shirika la mawasiliano la China Huawei pamoja na matumizi ya kijeshi ya Ujerumani, yote yakiwa masuala muhimu katika uhusiano kati ya washirika hao wanaopakana na bahari ya Atlantiki.
Kabla ya mazungumzo na Mike Pompeo leo, kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema:
"Tutajadili matatizo mbali mbali, dunia imo katika hali ya wasi wasi mkubwa, hususan suala la Iran na vipi tunaweza kuzuwia Iran kujipatia silaha za kinyuklia, vipi tutaweza kuzuwia hatua za kimabavu na uchokozi za Iran, tutazungumzia kuhusu Afghanistan, ambako wote tuna vikosi vya jeshi, tutazungumzia pia juu ya hali nchini Syria na bila shaka hali tete nchini Libya."
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas amesema licha ya kuwa Marekani haishiriki tena katika makubaliano na Iran, yanayofahamika kama mpango wa pamoja wa kuchukua hatua ama JCPOA, lengo lake ni hilo hilo. Pompeo yuko katika ziara ya mataifa manne ya Ulaya ambapo pia atafika nchini Uswisi, na Uholanzi, kabla ya kuungana na rais Trump katika ziara yake nchini Uingereza.