1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, China zakamilisha mazungumzo ya biashara

31 Julai 2019

Wajumbe wa China na Marekani wamefanya leo mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana tangu nchi hizo mbili zilipokubaliana kusitisha vita vya kibiashara mwezi uliopita

https://p.dw.com/p/3N3Wb
US-Handelsbeauftragter Lighthizer und Finanzminister Mnuchin treffen Chinas Vizepremier Liu in China
Picha: REUTERS/N. H. Guan

Marekani na China mpaka sasa zimewekeana ushuru wa kiwango cha juu kwenye bidhaa zao za thamani ya zaidi ya dola bilioni 360 katika mzozo wa pande mbili uliojikita kwenye masharti ya kuitaka China kudhibiti kinachodaiwa kuwa ni wizi wa teknolojia ya Marekani na kutoa ushindani sawa kwa makampuni ya Marekani.

Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Robert Lighthizer na Waziri wa Fedha Steven Mnuchin walisalimiana kwa kupeana mikono na kusemezana na Makamu Waziri Mkuu Liu He leo asubuhi.

Kikundi hicho kisha kikaingia katika mkutano wa faragha kwa karibu masaa manne katika mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana tangu Trump alipokubaliana kusitisha vita vya kibiashara na mwenzake wa China Xi Jinping mwezi Juni kufuatia kuporomoka kwa mazungumzo mwezi uliotangulia.

Handelsstreit zwischen China und den USA
Mvutano wa kibiashara wa China na Marekani umedumu mwaka mmojaPicha: AFP/Getty Images/G. Baker

Mazungumzo ya leo yalikuwa mafupi na wajumbe hao walijitokeza mapema kiasi kuliko ilivyotarajiwa, kwa ajili ya kupigwa picha ya pamoja kabla ya maafisa wa biashara wa Marekani kuelekea uwanja wa ndege bila kuzungumza na wanahabari.

Lighthizer na Mnuchin waliwasili mjini Shanghai jana na kuungana na maafisa wa China kwa chakula cha jioni na mazungumzo yasiyo rasmi – wakati tu Trump alipoingia kwenye Twitter kushambulia kile alichokisema ni ukosefu wa nia kutoka kwa China kufikia mkataba mzuri.

Aliandika kuwa na hapa namnukuu "timu yangu inafanya nao mazungumzo sasa, lakini kila mara wao hubadilisha muafaka huo mwishowe ili wanufaike,”. Mwisho wa nukuu. Trump aidha aliionya China dhidi ya kusubiri muhula wake wa kwanza umalizike ili kufikia muafaka wowote wa kibiashara, akisema kama atachaguliwa tena katika uchaguzi wa rais wa Novemba 2020, matokeo yake yatakuwa mabaya zaidi kwa China.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China Hua Chunying amesema Marekani inapaswa kulaumiwa kwa mazungumzo hayo yanayofanywa bila ya mafanikio kwa kipindi cha mwaka mmoja. Katika ripoti iliyochapishwa leo na shirika la habari la Xinhua, Ofisi ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya China imeonya kuhusu hatari mpya na kuongezeka kwa shinikizo la kuushusha uchumi wa China.

Wachambuzi wanasema kauli za Trump hazitasaidia kupunguza mahusiano tete ambayo tayari yapo kati ya Washington na Beijing