1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Biden asema bado yuko katika mbio za White House

29 Juni 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuwa bado yuko katika kinyang'anyiro cha Ikulu ya White House. Biden alizungumza katika mkutano wa kampeni katika jimbo muhimu la North Carolina Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4henx
Uchaguzi wa Marekani 2024
Biden alionekana mchangamfu North Carolina tofauti na alivyokuwa wakati wa mdahalo wa televisheniPicha: Evan Vucci/AP/dpa/picture alliance

Tangazo lake limejiri baada ya kukabiliana na Donald Trump katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais wa 2024 nchini Marekani. Katika hotuba yake ya dakika 18, Biden alionekana kuwa mchangamfu kuliko usiku uliotangulia wakati wa mdahalo huo wa televisheni.

Katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais wa msimu wa 2024, Biden alitoa majibu katika sauti yenye mkwaruzo na wakati mwingine kuonekana kupoteza mawazo yake. Katika jimbo la North Carolina, rais huyo wa Marekani alikiri namna vyombo vya habari vilizungumzia alivyofanya katika mdahalo huo.

Soma pia: Trump asema Wamarekani hawatokubali kifungo chake

Alisema yeye sio kijana tena na akakiri kuwa kwa sasa hafanyi vyema katika midahalo kama alivyokuwa akifanya huko nyuma. Hata hivyo, alisisitiza kuwa anajua jinsi ya kuchapa kazi. Matokeo mabaya ya Biden katika mdahalo wa Alhamisi usiku yaliwafanya baadhi katika chama chake cha Democratic kuhoji kama anapaswa kubadilishwa na tiketi hiyo kupewa mtu mwingine. Mchakato huo hauwezekani kwa urahisi isipokuwa kama Biden ataamua kujiondoa.