1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marcelo awaaga mashabiki wa Madrid

30 Mei 2022

Maelfu ya mashabiki wa Real Madrid walimiminika mitaani kuwalaki Madrid na kusherehekea ushindi wa timu yao wa Kombe la 14 la Ulaya, sherehe ambazo kilele chake kilikuwa ni dimbani Santiago Bernabeu.

https://p.dw.com/p/4C3IU
Champions-League-Finale - Liverpool vs. Real Madrid
Picha: Molly Darlington/REUTERS

Kumekuwa na tafrija tangu jana mchana wakati maelfu ya mashabiki wa Real Madrid walimiminika mitaani kuwalaki na kusherehekea ushindi wa timu yao wa Kombe la 14 la Ulaya, sherehe ambazo kilele chake kilikuwa ni dimbani Santiago Bernabeu. Madrid ilishinda 1-0 kupitia bao la Vinicius Jr.

Wachezaji waliolionyesha kombe hilo kwenye basi kubwa la wazi kwenye mitaa ya Madrid na walipofika uwanjani Bernabeu, nahodha Marcelo akatumia fursa hiyo kuwaaga mashabiki wa Real Madrid huku akibubujiwa na machozi. Nyota huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 34 amekuwa Real Madrid tangu 2007 na anaondoka baada ya kubeba kombe lake la tano la Ulaya. "Kutoka moyoni mwangu ningependa kukushukuruni kwa kuwa hapa kupokea makombe haya mawili. Pia nasema ahsante kwa Jumuiya ya Madrid, ambayo ni mji mzuri sana, na ni sisi tu tunaofahamu jinsi inavyopendeza kuishi hapa kwa miaka hiyo yote, na tumefurahia sana."

Mapema, rais wa Real Madrid Florentino Perez aliiambia timu hiyo sasa kuelekeza malengo yao katika kubeba Kombe la Ulaya 15 msimu ujao

Madrid sasa wameshinda mataji matano ya Ulaya katika miaka minane rekodi ambayo ni ya kipekee.

reuters, afp