1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marafiki wa Syria wakutana Paris

6 Julai 2012

Rais Francois Hollande wa Ufaransa ametaka vikwazo vikali zaidi viwekwe dhidi Rais Bashar al-Assad wa Syria na waasi wa nchi hiyo wapewe ushirikiano zaidi katika kumwondoa Assad madarakani.

https://p.dw.com/p/15SO2
Rais Francois Hollande akizungumza katika mkutano wa marafiki wa Syria
Rais Francois Hollande akizungumza katika mkutano wa marafiki wa SyriaPicha: dapd

Akizungumza katika mkutano wa kundi linalojiita marafiki wa Syria unaofanyika mjini Paris, Ufaransa, Hollande alisema kwamba rais Assad ni lazima aondoke madarakani. Rais huyo aliwaambia mawaziri wa mambo ya kigeni pamoja na wanadiplomasia wanaohudhuria mkutano huo kwamba hatua ya kumwondoa Asad madarakani itakuwa na faida kwa Syria, majirani zake pamoja na kwa kila mtu anayetaka amani ipatikane katika eneo hilo.

Hollande amewaomba washiriki wa mkutano wakubaliane na uamuzi wa kuongeza kiasi cha msaada wa kibinadamu kinachopelekwa Syria. Mwenzake wa Marekani, Hillary Clinton, amezilaumu China na Urusi ambazo hazishiriki katika mkutano wa leo na amesema kuwa nchi hizo zitawajibika kwa kuuunga mkono utawala wa Assad. Clinton amerudia pia kuutaka Umoja wa Mataifa uiwekee Syria vikwazo zaidi.

Hillary Clinton na Guido Westerwelle katika mkutano
Hillary Clinton na Guido Westerwelle katika mkutanoPicha: dapd

Wafuasi wa al-Qaeda waingia Syria

Muda mchache kabla ya kuanza kwa mkutano huo kuhusu Syria, waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, amesema kwamba Marekani, Urusi na Ufaransa hazitakuwa tayari kumpa Assad hifadhi ya kisiasa. "Swali ni kama lipo taifa lililo tayari kumpokea Assad lakini inaelekea kwamba Urusi, Marekani, Ufaransa na labda hata China haziko tayari kumpokea. Hili ni swala linalopaswa kushughulikiwa," alisema Fabius kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Europe 1.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, jana alithibitisha kwamba baadhi ya nchi za Magharibi zimeiomba Urusi impe Assad hifadhi ya kisiasa lakini Lavrov amesema kuwa nchi yake ililichukulia ombi hilo kama utani.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei LavrovPicha: picture-alliance/dpa

Naye Hoshyar Zebari, ambaye ni waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, ameeleza kwamba utawala wa nchi yake unahofia kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda wanaelekea Syria kwenda kufanya mashambulizi huko. Magaidi hao wanautumia wakati huu ambapo kuna hali ya vurugu Syria kuingia nchini humo.

WikiLeaks kuchapisha barua pepe kutoka Syria

Wakati hayo yakiendelea, nchini Syria kwenyewe, mkuu wa kitengo maalum cha jeshi la nchi hiyo kinachomlinda rais, Republican Guard, na mshirika wa muda mrefu wa Rais Assad, Brigedia Jenerali Manaf Tlas, ametoroka na sasa yuko njiani kuelekea Paris. Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa familia ya Tlas, Jenerali huyo aliwasili nchini Uturuki hapo jana na sasa anakwenda kujiunga na baba yake anayeishi Ufaransa, Mustafa Tlas, ambaye aliwahi kuwa waziri wa ulinzi wa Syria.

Nayo tovuti ya WikiLeaks inayofahamika kwa kuchapisha nyaraka za siri katika mtandao wa internet, imetangaza kwamba iko katika mchakato wa kuchapisha barua pepe millioni 2.4 kutoka Syria, sehemu kubwa zikiwa zimeandikwa na maafisa wa serikali ya nchi hiyo.

WikiLeaks inafahamika kwa kuchapisha nyaraka za siri
WikiLeaks inafahamika kwa kuchapisha nyaraka za siriPicha: picture-alliance/dpa

Mwanzilishi wa tovuti ya WikiLeaks, Julian Assange, amekaririwa akisema kuwa taarifa zilizoandikwa katika barua pepe hizo zitaiaibisha Syria na vile vile kuyaaibisha mataifa yanayoipinga Syria. Msemaji wa tovuti hiyo, Sarah Harrison, amemleza kuwa nyaraka zitakazochapishwa zinaonyesha kwamba pamekuwa na ushirikiano baina ya serikali ya Syria na makampuni ya nchi za Magharibi.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/reuters/afp/ap

Mhariri: Mohammed Khelef