Mar del Plata, Argentina. Mkutano wamalizika bila makubaliano.
6 Novemba 2005Mkutano wa mataifa ya Amerika umemalizika bila ya kupatikana makubaliano ya kusukuma mbele mpango unaoungwa mkono na Marekani wa kulifanya eneo la kusini na kaskazini ya Amerika kuwa ni eneo moja la biashara huria.
Maafisa wa Marekani wamesema kuwa mataifa 29 kati ya 34 yaliyowakilishwa katika mkutano huo uliofanyika katika mji wa kitalii wa Mar del Plata nchini Argentina wanaunga mkono mpango huo wa kuundwa kwa kile kitakachojulikana kama eneo la biashara huria la Amerika , ama FTAA.
Lakini rais wa Venezuela Hugo Chavez ameongoza upinzani dhidi ya mapendekezo hayo. Siku ya Ijumaa, aliuambia mkutano unaopinga biashara huria katika uwanja wa mpira kuwa anania ya kuuzika mpango huo.
Mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku mbili, ulishuhudia maandamano makubwa dhidi ya sera za Marekani.