1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tahriri

15 Januari 2011

Nchini Tunisia, maandamano ya Umma yameweza kumuondoa rais wa nchi madarakani, hatua ambayo ilisubiriwa kwa muda mrefu na yenye maana kubwa kwa eneo zima la Afrika ya Kaskazini na nchi za Kiarabu.

https://p.dw.com/p/zy5J

Hii ni hatua kubwa ya kihistoria na alama ya namna ambavyo raia wana nguvu gani dhidi ya tawala za kiimla na za kifisadi. Ni sauti inayosema wazi kwamba kubadilisha utawala kunaweza kufanyika bila ya vita - bila ya uingiliaji kati wa kijeshi, liwe la ndani au la nje, na bila ya hata uongozi wa wanasiasa wa upinzani au wanaharakati wa taasisi za kiraia.

Tayari tangu mwanzoni kabisa, kupitia blogu za Kiarabu na majukwaa mengine ya mtandaoni, kulishaonekana sauti za kuwaunga mkono vijana wa Kitunisia, ambao walikuwa wakiupa onyo utawala wa nchi yao. Vijana hawa walikuwa wameshachoka na mfumo wa kidhalimu, ufisadi uliopindukia mipaka na ukosefu mkubwa wa ajira, mambo ambayo yamekuwa utaratibu wa kawaida kwenye nchi za eneo hili.

Jamii inapokuwa na mambo kama hayo, matokeo yake huwa ni hasira na ghamidha dhidi ya mfumo wa maisha uliofeli na mwisho wake ni bomu linaloripuka na kuzalisha mgogoro katika eneo zima.

Na wala Tunisia si mfano pekee, bali hivyo ndivyo zilivyo jamii karibuni zote katika nchi za Kiarabu. Na kwa kuwa mote humo, vijana ndio wanaofanya asilimia kubwa ya wakaazi wake, na hiyo maana yake ni kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa matukio kama haya kujirejea. Katika siku za karibuni, kumekuwa pia na maandamano katia nchi za Algeria, Jordan na Misri. Na bado nchi nyengine zinafuatia.

Inawezekana ikawa bado ingali mapema mno kuiita hatua hii ya vijana wa Tunisia kuwa imeweza kuwapa kile hasa wanachokitaka, lakini lazima isemwe kuwa wameonesha njia kwa vijana wenzao wa nchi za Kiarabu. Kwa hatua hii, Tunisia inasimama kama kigezo cha namna ambavyo demokrasia inaweza kupatikana, bila ya shaka na gharama pia ambazo demokrasia hiyo inaweza kulipiwa.

Kwa kila hali, mapinduzi haya ya Tunisia yanachukuwa dhamana ya kuwa alama ya mapambano dhidi ya tawala, ambazo zinapingana na uwazi, demokrasia na haki za binaadamu. Mapinduzi haya yanapaza sauti kwamba, zama za uhuru, ushindani wa kidemokrasia na haki ndio zimefika, na japokuwa njia ya kufikia huko si rahisi, lakini si kuwa haiwezekani.

Bara la Ulaya, likiwa ni jirani wa nchi za Kaskazini ya Afrika na ulimwengu wa Kiarabu, ni lazima lipate funzo kupitia hali ya mambo inavyoendelea nchini Tunisia. Na muhimu kuliko yote ni kuwa: hatupaswi kuziba masikio na macho yetu, pale tawala za nchi hizo, ambazo kwa bahati mbaya pia ni marafiki zetu, zinapopondaponda haki za binaadamu au kuharibu chaguzi, kama ulivyo mfano wa Misri. Mfano huu wa Tunisia unatwambia kuwa, utawala wa kiimla unaweza tu kuwa na amani ya kitambo.

Mwandishi: Rainer Sollich/ZPR/Mohammed Khelef

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman