1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yasitishwa Ukraine kuruhusu raia kuondoka

9 Machi 2022

Juhudi za kuwaondoa maelfu ya watu waliokwama kwenye mazingira hatari yanayokumbwa na mashambulizi nchini Ukraine zinaendelea huku mataifa ya magharibi yakitafakari hatua ziada kuisaidia Ukraine kwenye mzozo na Urusi.

https://p.dw.com/p/48Eui
Ukraine-Konflikt | Zivilisten fliehen aus Sumy
Picha: Ukrainian Presidency/AA/picture alliance

Mapema leo Jumatano mamlaka za Ukraine zilitangaza kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kuwaruhusu raia kuondoka kwenye miji ya Mariupol na Sumy iliyo Kaskazini Mashariki, mji wa Enerhodar huko Kusini na Volnovakha unaopatikana Kusini Mashariki.

Maeneo mengine pia karibu na mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, yalitarajiwa kushuhudia usitishaji mapigano ili kutoa nafasi ya watu kukimbia vita.

Mashambulizi ya siku kadhaa mfululizo huko katika mji wa Mariupol yalitatiza mawasiliano baina ya wakaazi wa mji huo na maeneo mengine ya nchi hiyo huku wengine ya raia wakihangaika kutafuta maji na vyakula.

Juhudi za hapo kabla za kufungua maeneo salama ya kuwezesha raia kuondoka zilishindikana kutokana na mashambulizi ya Urusi na hadi hivi leo bado haijafahamika iwapo hatua mpya zilizochukuliwa zimewezesha watu waliokwama kuondoka maeneo yenye mapigano.

Mzozo huo ulionza wiki mbili zilizopita baada ya rais Vladimir Putin kuamuru jeshi lake kuingia Ukraine unatazamiwa kuzidi makali wakati huu jeshi la Urusi likizidisha mashambulizi kujibu upinzani mkali inaopata kutoka wapiganaji wa Ukraine.

Mataifa ya EU yaongeza vikwazo dhidi ya Urusi 

Wakati hayo yakijiri mataifa ya Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuongeza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi kutokana na hatua ya Moscow kuivamia kijeshi Ukraine.

Frankreich Strassburg | Flaggen der Ukraine und Europa am Europaparlament
Picha: Pascal Bastien/AP/picture alliance

Kanda hiyo ya mataifa 27 imeidhinisha mkururo wa vikwazo ziada vikiwalenga viongozi mjini Moscow,  mabwenyenye wa kirusi na familia zao pamoja na mabenki ya Belarus, ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi.

Umoja wa Ulaya pia umeridhia vikwazo vinavyoilenga sekta ya bahari. Maaumzi hayo yamefikiwa kuelekea mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika kesho huko Versailles nchini Ufaransa ambapo suala la utegemezi wa mkubwa wa nishati inayotoka Urusi barani Ulaya litakuwa ajenda ya juu ya majadiliano.

Uingereza na Canada kupelekea msaada wa silaha nchini Ukraine 

Kwa upande wake Uingereza imesema inapanga kuipatia Ukraine mifumo ya kisasa ya kudungua ndege za kivitia kuisaidia nchi hiyo kulinda anga yake dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Flugabwehrrakete Strela
Picha: Konstantin Mihalchevskiy/Sputnik/SNA/imago images

Mipango hiyo imetangazwa na waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallice na iwapo itaidhinishwa itakuwa ni hatua kubwa ya msaada wa kijeshi kutoka mataifa ya magharibi. 

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau aliye ziarani nchini Ujerumani amesema amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais Prime  Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine na kumwarifu kuwa Canada itatuma vifaa vya kisasa vya ulinzi katika siku chache zinazokuja. Trudeau pia amesema amemwalika Zelensky kuhutubia bunge la Canada hivi karibuni.

Katika hatua nyingine makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris anakwenda Poland leo saa chache tangu Washington ilipokataa pendekezo la nchi hiyo la kuipatia Ukraine  ndege zake zote za kivita chapa Mig-29 kupitia kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Ujerumani.

Harris amepangiwa kukutana na viongozi wakuu wa Poland ambapo pamoja na mambo mengine atawashukuru kwa msaada ambao nchi hiyo inatoa kuwasaidia wakimbizi wa Ukraine.