Mapigano yapamba moto Homs
1 Julai 2013Mapigano yanayoendelea tangu siku tatu zilizopita kati ya waasi na vikosi vya serikali yanaripotiwa pembezoni mwa mitaa inayodhibitiwa na waasi-linasema shirika linalosimamia haki za binaadam na kuongeza wapiganaji wa Hisbollah wanashirikiana na wanajeshi wa serikali,kama ilivyotokea katika mapambano ya kuukomboa mji wa Qusseir,mwezi kama mmoja hivi uliopita.
"Hujuma za mabomu dhidi ya maeneo ya waasi huko Homs,zinaendelea kwa nguvu lakini jeshi halisongi mbele na hadi sasa limeshindwa kuliteka hata eneo moja."Mkurugenzi wa shirika hilo la haki za binaadam lenye makao yake makuu nchini Uingereza,Rami Abdel Rahmane amesema.
Vikosi vya serikali ya rais Bashar al Assad vinauzunguka mtaa wa Khalidiye,kaskazini ya Homs na katika eneo la mji wa kale,linasema shirika hilo linalojipatia habari zake toka duru za hospitali na wanamgambo.
"Mapigano yanaendelea katika mitaa hiyo na jeshi na washirika wao wameshapoteza watu 32 mnamo muda wa siku mbili" ameongeza kusema Abdel Rahmane.
Homs mji muhimu kimkakati
Homs, wenyewe waasi wanauita "mji mkuu wa mapinduzi" ni mjimuhimu kimkakati kwasababu unakutikana katikati ya Syria na unaliunganisha eneo la kaskazini na lile la kusini la nchi hiyo.
Kwengineko nchini humo vikosi vya serikali vinaendelea kuhujumu maeneo ya karibu na mji mkuu Damascus;lengo kuu likiwa kambi ya wakimbizi wa kipalastina ya Yarmuk kusini mwa Damascus,Qabun,katika eneo la mashariki na Daraya,kusini mashariki.
Baraza la usalama latakiwa likutane haraka
Viongozi wa baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba wameitolea wito baraza la usalama la Umoja wa mataifa likutane haraka na kupitisha uamuzi ili kuzuwia mauwaji katika mji wa Homs.Katika taarifa yao viongozi hao wa mataifa sita ya kifalme ya Ghuba wamesema "wanafuatilizia kwa hofu kuzingirwa mji wa Homs" na vikosi vya serikali ya Syria na wanamgambo wa Hisbollah.
Wakatai huo huo shirika la haki za binaadam Human Rights Watch linalalamika na kusema nchi jirani na Syria,ikitengwa Libnan,zinawawekea vizuwizi wakimbizi wanaotaka kuingia katika nchi hizo.
Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa mzozo wa Syria ulioripuka tangu March mwaka 2011 umesababisha watu milioni moja na laki saba kuyahama maskani yao.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri :Yusuf Saumu