Mapigano yamepamba moto nchini Côte d'Ivoire
29 Machi 2011Miji hiyo miwili ilikuwa hapo awali ikidhibitiwa na vikosi tiifu kwa Laurent Gbagbo.Mapigano hayo ya kunyakua maeneo ya magharibi karibu na mpaka wa Liberia yameanza mwishoni mwa mwezi wa Feburary.
Kutekwa miji hiyo miwili ya Daloa na Doékoué, inayokutikana katika njia panda kati ya mji mkuu wa kisiasa Yamoussoukro na mji muhimu wa bandari San Pedro,ni muhimu kwa vikosi vya Ouattara ili kuweza kudhibiti kitovu cha shughuli za kusafirisha Cacao.
Mapigano haya mepya yameripuka katika wakati ambapo hali inazidi kuwa mbaya huku malaki ya wa-côte d'ivoire wakiyapa kisogo maskani yao.
Jacques Francuin wa shirika la Umoja wa mataifa linalowahudhumia wakimbizi amesema:
"Tunakadiria watu kati ya laki sabaa na laki nane wameshayapa kisogo maskani yao mjini Abidjan.Pengine zaidi.Ni shida kutoa picha halisi ya mambo,kwasababu hatuwezi kutoka.Wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wanaangaliwa kama adui humu nchini."
Wapiganaji wa Forces Republicaines,kama wanavyojulikana hivi sasa wanamgambo wanaomuunga mkono Alassane Ouattara wanasemekana wameuteka pia mji wa mashariki Bondoukou unaopakana na Ghana..
"Watu wametoka nje na kushangiria" shahidi mmoja amesema.Duru za Forces Republicaine zinasema wapiganaji nwao wanaelekea Tanda,kusini mwa Côte d'Ivoire.
Umoja wa mataifa unakadiria watu wasiopungua 462 wanasemekana wamepoteza maisha yao,wengi wao ni raia wa kawaida,tangu mgogoro wa Côte d'Ivoire uliporipuka mwishoni mwa mwezi wa November mwaka jana.Lakini kambi ya Alassane Ouattara inaamini waliouwawa hawajapungua watu 832.
Hatima ya mgogoro huo haijulikani,na juhudi za kusaka ufumbuzi wa kisiasa mpaka sasa hazikuleta tija.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp/Reuters
Mhariri:Abdul-Rahman