1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mapigano yaendelea Sudan

22 Aprili 2023

Mapambano ya kugombea madaraka ya nchi kati ya vikosi tiifu kwa mkuu wa majeshi ambaye pia ni mtawala mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na vile vinavyomtii naibu wake Mohammedi Hamdan Dagalo yameendelea.

https://p.dw.com/p/4QQrN
Sudan Khartum | Rauch in der Nähe des Doha International Hospital
Picha: Maheen S/AP/dpa/picture alliance

Licha ya pande mbili hasimu za jeshi kutangaza kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu za sikukuu ya Eid el Fitr, mapigano yameendelea sehemu mbalimbali katika mji wa Khartoum na katika mji jirani wa Nile, na hivyo kukwamisha juhudi za kimataifa.

Milio ya risasi na milipuko ya mabomu vilisika huku mashambulizi ya anga pia yakiendelea. Uwanja wa ndege wa  Khartoum   haujaepuka athari za mapigano hayo. Mataifa kadhaa yakiwemo Marekani, Japan, Korea Kusini, Ujerumani na Uhispania hayakufanikiwa kuwahamisha raia na wafanyakazi wa balozi zao.

Washington imetangaza bila kutoa maelezo zaidi kuwa raia wake mmoja ameuawa huko Sudan na kwamba hadi sasa hakuna uamuzi wowote uliochukuliwa wa kuanzisha operesheni ya kuwaondoa wanadiplomasia wa Marekani huko Sudan, lakini Ikulu ya White House imesisitiza kuwa wanajiandaa kwa operesheni hiyo.

Soma pia: Mataifa zaidi kuwaondoa raia wao Sudan

Takriban wafanyakazi watano wa mashirika ya kutoa misaada wameuawa, wakiwemo watatu kutoka kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Tangu wakati huo Shirika hilo la kimataifa limesitisha kwa muda shughuli zake nchini Sudan, ikiwa ni moja ya operesheni kubwa zaidi ya msaada wa chakula duniani.

WFP imesema ghasia hizo zinaweza kuwatumbukiza katika njaa mamilioni ya waSudan, katika nchi ambayo watu milioni 15 ikiwa ni sawa na thuluthi moja ya raia wanahitaji msaada huo.

Mapigano yaendelea kusababisha maafa makubwa

Sudan Khartum | Kämpfe | zerstörtes Militärfahrzeug
Gari ya jeshi iliyoharibiwa kwa kombora kusini mwa jiji la Khartoum, SudanPicha: Marwan Ali/AP Photo/picture alliance

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limesema angalau watu 413 wameuawa na maelfu ya wengine wamejeruhiwa wakati ambapo hospitali zikikabiliwa pia na mashambulizi. Shirika hilo limeendelea kuwa watu wapatao 20,000 wamekimbilia nchi jirani ya Chad,   na kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi na nishati imezidi kuongezeka.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, limesema hatua za haraka zinahitajika ili kusitisha ghasia zinazoweza kugeuka kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, na kuonya kwamba hali ya kutisha ambayo wengi waliihofia nchini Sudan ndiyo inayoshuhudiwa kwa sasa.

Sudan ambayo ni nchi ya tatu kwa ukubwa barani Afrika, inapakana na nchi saba ikiwemo Misri, Saudi Arabia, Ethiopia na eneo tete la Sahel. Ghasia zinazoendelea nchini humo zinahatarisha kuendelezwa kwa mivutano ya kikanda.