1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mapigano yaendelea kati ya jeshi la Urusi na Ukraine Soledar

11 Januari 2023

Mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine leo Jumatano katika mji wa Soledar, mashariki mwa Ukraine, uliokuwa na idadi ya watu wapatao 10,000 kabla ya vita hivyo.

https://p.dw.com/p/4M1Yt
Salzmine Soledar Ukraine
Picha: Alex Chan/ZUMA/IMAGO

Kushamiri kwa mashambulizi katika mji huo kunatajwa kama hatua ya Urusi kutaka kulikamata kabisa eneo zima la Donbas na iwapo itafanikiwa kuutia mkononi mji huo, itakuwa kama alama ya mafanikio baada ya Moscow kuonekana kushindwa na Ukraine katika uwanja wa mapambano katika miezi ya hivi karibuni.

Soma pia: Urusi yaushambulia mji wa Kharkiv baada ya ziara ya Baerbock

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kuwa jeshi lake la anga limeuzingira mji wa Soledar na kukata njia za mawasiliano kutoka upande wa kaskazini na kusini. Msemaji wa wizara hiyo ya ulinzi Igor Konashenkov amesema, "Katika muendelezo wa mashambulizi kuelekea eneo la Donetsk, vikosi vya Urusi vimeyakomboa makaazi ya Pidhorodne katika jamhuri ya watu wa Donetsk. Jeshi letu la anga limekata njia za mawasiliano za upande wa kaskazini na kusini mwa mji huo. Jeshi limefanya mashambulizi dhidi ya ngome za adui."

Katika taarifa yake ya kila siku kuhusu vita hivyo, wizara ya ulinzi imesema wanajeshi wa Urusi wanaendelea na mapambano kuchukua udhibiti kamili wa Soledar, mji mdogo katika eneo la mashariki la Donetsk ambao umekuwa kiini cha mashambulizi katika miezi kadhaa sasa.

Ukraine yakanusha kuwa mji wa Soledar uko chini ya udhibiti wa Urusi

Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten in Soledar
Kamanda wa jeshi la Ukraine Kanali Oleksandr Syrskyi akitoa maelekezo kwa wanajeshi wake katika mji wa SoledarPicha: Roman Chop/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, Ukraine imekanusha kuwa mji huo, uliokuwa na idadi ya watu wapatao 10,000 kabla ya vita hivyo, umeingia mikononi mwa jeshi la Urusi.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar ameandika katika mtandao wake wa Telegram kuwa, "mapigano makali yanaendelea Soledar."

Bi Maliar ameendelea kueleza kuwa "adui amevibadilisha vitengo vyake tena baada ya kupata hasara, na kwamba ameongeza wapiganaji wake wa Wagner ili kujaribu kuchukua udhibiti wa mji huo japo wamepatana na kizingiti."

Kundi la mamluki la Wagner ambalo limeongoza mashambulizi hayo, jana lilidai kuchukua udhibiti wa mji huo wa madini ya chumvi japo wanajeshi wa Ukraine walikuwa bado hajawakata tamaa kuuachilia mji huo.

Soma pia: Urusi yadai kukiteka kijiji karibu na Bakhmut

Shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha jinsi hali ilivyo katika mji huo wa Soledar lakini mpiga picha wake aliyefika katika viunga vya mji huo siku chache zilizopita amesema wakaazi wengi wameukimbia mji huo.

Mpiga picha huyo ameeleza kuwa aliona moshi na kusikia milio ya risasi.

Kuukamata mji wa Soledar kutatafsiriwa kama alama ya mafanikio baada ya Moscow kuonekana kushindwa katika uwanja wa mapambano katika miezi ya hivi karibuni.

Zelensky atoa heshima kwa wanajeshi wa Ukraine waliopoteza maisha vitani

Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihutubia waandishi wa habariPicha: AFP/Getty Images

Wakati hayo yanaripotiwa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa heshima zake za mwisho kwa wanajeshi waliozikwa wakati wa ziara yake katika mji wa magharibi wa Lviv leo Jumatano. Zelenskiy, maafisa wa mji huo na mkuu wa wafanyikazi Andrii Yermak walishiriki hafla ya kuwakumbuka wanajeshi waliouawa vitani tangu kuanza kwa vita hivyo Februari mwaka uliopita.

Soma pia: Urusi yakiri kupoteza zaidi ya wanajeshi 60

Kiongozi huyo baadaye alifanya mkutano na makamanda wa kijeshi ambapo kando na mambo mengine, walijadiliana juu ya juhudi za ulinzi wa mipaka na hali ya usalama kaskazini magharibi mwa Ukraine.

Zelensky amesema Ukraine lazima iwe macho katika mpaka wake na mshirika wa Urusi, Belarus licha ya kuona kile alichosema "kauli zenye nguvu" kutoka kwa jirani yake.

Kiev imetahadharisha kuwa Urusi inaweza kujaribu kuitumia Belarus kama ngazi ya kuanzisha mashambulizi ya ardhini kutoka upande wa kaskazini mwa Ukraine.