Mashambulizi yaendelea Syria licha ya tangazo la Urusi
28 Februari 2018Siku tisa baada ya vikosi vya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi kuongeza mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi, makubaliano ya kusitisha mapigano yaliwapa matumaini raia ambao walikuwa wakijificha kwenye vyumba vya chini vya nyumba zao.
Lakini siku ya kwanza ya usitishwaji mapigano wa masaa matano ulioamrishwa Jumatatu na Rais Vladimir Purtin wa Urusi na kuanza saa tatu asubuhi iligubikwa na vurugu zilizosababisha watu saba kuuawa.
Serikali ya Syria kwa upande wake imejitetea kwa kusema inachokifanya Ghouta Mashariki ni kuwakomboa wananchi kutoka katika ukatili wa makundi ya kigaidi.
"Haya ni makundi ya kigaidi, hawajali watu, hawajali watoto, wanajaribu kupotosha maoni ya umma wa kimataifa. Tunachojaribu kufanya ni kuwakomboa watu wa Ghouta Mashariki kutokana na makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa huko kwa miaka sita hadi saba iliyopita," amesema Faisal Mikdad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria.
Mashambulizi bado yanaendelea siku ya pili ya kutangazwa kusitishwa
Na siku ya Jumatano vikosi vya serikali ya Syria vimeripotiwa kudhibiti maeneo kadhaa mashariki mwa Ghouta vikishirikiana na makundi ya wanamgambo katika mapigano dhidi ya waasi, licha ya mpango wa Urusi wa kusitisha mapigano.
Jumanne ambayo ilikuwa siku ya mwanzo ya makubaliano hayo, Urusi ilionekana kushindwa kutimiza lengo lake la kusitisha mapigano ikiwa ni mpango unaotegemewa kuendelea kwa siku 30 zijazo, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa katika Braza la Usalama la Umoja wa Mtaifa. Waaazi 400,000 wa eneo hilo pia wameonekana kukosa imani nao mpango huo.
Tangazo hilo la kusitishwa mapigano kwa masaa matano halikuleta amani yoyote Mashariki mwa Ghouta.
Mashambulizi ya mabomu yalifanyika katika eneo la Jisreene na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na kujeruhi wengine 17, kulingana na Shirika linalofuatilia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza.
Shirika hilo limeongeza kuwa mashambulizi mengine kadhaa yalishuhudiwa katika maeneo ya Ghouta Mashariki kama vile lKfar, Batna na Arbeen kabla ya muda wa kusitisha mapigano kumalizika. Usitishwaji mapigano uliosimamiwa na Urusi ulianza saa tatu asubuhi na kumalizika saa nane mchana.
"Usitishwaji mashambulizi ulikuwa ni wakuchekesha. Waliambiwa ni usitishwaji mapigano wa kuruhusu kuingizwa misaada ya kiutu lakini waliwaruhusu washirika wao kurusha mabomu na kufanya mashambulizi ya anga," amesema Daktari Mohammed kutoka Ghouta Mashariki.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana Jumatano mchana kujadili hali ya kibinadamu nchini Syria na litazungumza na kumsikiliza mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/dpa/afp
Mhairiri: Mohammed Khelef