Mapigano yaanza tena Sudan baada ya makubaliano ya saa 24
11 Juni 2023Makubaliano ya karibuni ya kusitisha mapigano yaliwawezesha raia waliokwama mjini Khartoum kuondoka nje ya majumba yao na kununua vyakula na bidhaa nyingine muhimu.
Lakini kwa mujibu wa mashuhuda, dakika kumi tu baada ya mpango huo kumalizika saa kumi na mbili kamili asubuhi ya leo mji huo mkuu ukakumbwa tena na milio mikubwa ya makombora na risasi.
Soma pia:
Walioshuhudia wamesema makombora mazito yalivurumishwa katika mji wa Khartoum na mji pacha wa Omdurman katika upande wa kaskazini, na mapigano yakazuka tena kwenye Mtaa wa Al-Hawa, kusini mwa Khartoum.
Mapigano makali yameikumba nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika tangu katikati ya Aprili, wakati mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo, anayeongoza kikosi cha Rapid Support Forces - RSF, kuanza kuzozana.