1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano makali yazuka Tripoli

Isaac Gamba
16 Januari 2018

Mapigano makali yamezuka katika mji mkuuu wa Tripoli, Libya na kusababisha kiasi ya watu 20 kuuawa, kufungwa kwa uwanja wa ndege pamoja na kuharibu ndege.

https://p.dw.com/p/2qtx6
Libyen Tripolis Platz der Märtyrer Stadtbild Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/M. Turkia

Shambulizi hilo liliibua mapigano makali ambayo yamekuwa yakitikisa mjini Tripoli miezi kadhaa na kuyayeyusha madai ya serikali inayotambuliwa kimataifa ya kuwa imerejesha uthabiti katika mji huo. Vurugu hizo pia zinakwamisha juhudi za serikali inayotambuliwa kimataifa kushawishi balozi mbalimbali kurejesha shuhguli zake katika mji huo.

Milio ya risasi pamoja na milipuko ilisikika katika mji wa Tripoli mapema hapo jana na maafisa   katika  uwanja wa ndege wa Mitiga unaosimamia safari za ndege za kiraia wanasema  safari za ndege katika uwanja huo zimesimamishwa hadi itakapo tangazwa tena.

Uwanja huo ulionekana kuwa tupu majira ya alasiri hapo jana wakati mapigano yalipo kuwa yamemalizika ingawa marubani walipeleka ndege katika uwanja wa ndege wa kimataifa uliofungwa tangu mwaka 2014 kwa lengo la kuhakikisha ulinzi wa ndege hizo  kutokana na uwanja huo kuharibiwa  wakati wa mapigano yaliyotokea awali.

 Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Reuters alishuhudia ndege aina ya Airbus chapa A319 iliyoko chini ya shirika la ndege la Afriqiya ikiwa imeegeshwa katika uwanja wa ndege wa Mitiga huku ikiwa na tundu upande wa juu lililosababishwa na shambulizi.

Ndege nne nyingine nazo zilipata madhara kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni  shambulizi la risasi ikiwa ni pamoja na ndege mbili zilizoko chini ya shirika la ndege la Libya pamoja na ndege aina ya Boeing chapa 737 ambayo inaelezwa ilikuwa inatarajia kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo.

Mapigano yahusisha kikosi chenye nguvu kijulikanacho kama Rada

 Mapigano hayo yalihusisha moja ya kikosi chenye nguvu  nchini humo kijulikanacho kama Rada kilichopambana dhidi ya kikosi hasimu kilichoko katika mji wa jirani wa Tajoura.

Libyen Polizist in Tripoli
Picha: Reuters/I. Zitouny

Kikosi hicho cha Rada kinatumika kupambana dhidi ya uhalifu na ugaidi  pamoja  na kudhibiti usalama kwenye  uwanja wa ndege wa Mitiga na gereza lililoko jirani na uwanja huo.

Kikosi cha Rada kina mafungamano na serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa  na mara nyingi kimekuwa kikishambuliwa na makundi hasimu ambayo wapiganaji wake kimewatia nguvuni.

Kwa mujibu wa kikosi cha Rada uwanja wa ndege umeshambuliwa na wapiganaji ambao ni watiifu kwa kiongozi wa wanamgambo ajulikanaye kama Bashir pamoja na wapiganaji  wengine ambao wamekuwa wakitafutwa ambao walitoweka katika gereza lililoko mjini Tripoli ambalo kikosi hicho kinalidhibiti.

  Katika taarifa yake serikali inayotambuliwa kimataifa imesema shambulizi hilo lililolenga kuwaachia huru wanamgambo wa  kundi la itikadi kali linalojiiita Dola la Kiisilimu, wanamgambo wa al- Qaeda pamoja na wanamgambo wenye mafungamano na makundi mengine limeathiri usalama katika sekta ya anga  pamoja na kuleta hofu kwa raia.

Wizara ya afya nchini humo imesema kiasi ya watu 20 wameuawa katika mapambano  na wengine 60 kujeruhiwa wakiwemo raia.

Mitiga ni kambi  ya anga ya jeshi iliyoko jirani na mji wa Tripoli ambayo imekuwa ikiruhusu kutua kwa ndege za kiraia tangu  uwanja wa ndege wa kimataifa uliposimamishwa kutumika mwaka 2014.

Katika gereza lililoko jirani kikosi cha Rada kimesema  kinawashikilia watu 2,500 wakiwemo washukiwa wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre

Mhariri : Bruce Amani