1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Kundi la Hamas na Fatah/ Palastine

Mutasa Omar14 Juni 2007

Hamas wanakurubia kulidhibiti eneo zima la Gaza wakiwashinda nguvu wanajeshi wa usalama watiifu kwa rais Mahmoud Abbas anaepanga kuivunja serikali inayodhibitiwa na Hamas.

https://p.dw.com/p/CHCd
Ismael Haniya mkuu wa kundi la Hamas akizungukwa na walinzi wake
Ismael Haniya mkuu wa kundi la Hamas akizungukwa na walinzi wakePicha: AP

Wanaharakati waliobeba silaha nzitonzito waHamas wameliteka jengo muhimu la shughuli za usalama huko Gaza,kufuatia mapigano makali yaliyogharimu maisha ya watu 14 na kuwajeruhi wengine 70 hii leo.Hilo ni jengo la pili muhimu la usalama huko Rafah kutekwa na wanaharakati wa Hamas wanaojiandaa kuliteka jengo la tatu huko Beit Lahya,kaskazini mwa Gaza.

Jumla ya wapalastina 20 wameuliwa katika mapigano ya leo kati ya pande hizi mbili zinazohasimiana-na kuifanya jumla ya watu waliopoteza maisha yao kufikia 103 tangu mapigano haya yaliporipuka upya June sabaa iliyopita.

Wanamgambo wa Hamas wameyavamia pia makao makuu ya idara ya usalama katika mji wa Gaza na kuwataka watumishi wa jengo hilo wasalim amri.

Televisheni ya Hamas imeonyesha picha za watumishi wa idara ya usalama wanaolihama jengo hilo mikono juu, wakisimamiwa na wanaharakati wa kiislam waliojifunika nyuso zao.

Bendera ya Hamas yenye rangi ya kijani inapepea juu ya jengo lililoko katika mtaa uliobadilishwa jina na kuitwa Tal al Islam-badala ya tal al Hawa.

Katika taarifa yao, tawi la kijeshi la Hamas limesema limegundua nyaraka ndani ya jengo hilo zinazothibitisha kwamba watumishi wa idara za usalama wanashirikiana na maadui wa kizayuni kwa lengo la kutaka kuwauwa wakuu wa Hamas.

Katika wakati ambapo mapigano yamepamba moto huko Gaza,kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina, Mahmoud Abbas anashauriana pamoja na washirika wake wakuu, uwezekano wa kuivunja serikali ya umoja inayodhibitiwa na Hamas.

Mshauri wake,SAIEB ERAKAT amesema:

“Lengo letu ni kuona mapigano yanakoma.Tukishindwa,na ikiwa wamisri hawatafanikiwa katika juhudi zao za kutaka silaha ziwekwe chini,naamini rais,katika muda wa masaa machache yajayo atapitisha maamuzi ili kurejesha sheria na nidhamu kwa lengo la kuhifadhi umoja wa wapalastina.”

Kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palastina imemsihi rais Mahmoud Abbas aivunje serikali,kufuatia mkutano wa dharura aliokua nao hii leo mjini Ramallah.

Kamati kuu hiyo imemtaka pia rais wa utawala wa ndani atangaze sheria ya hali ya hatari katika maeneo ya utawala wa ndani na kuunda serikali ya dharura .Kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palastina imemtaka pia rais Abbas aombe hifadhi ya kimataifa na kulitangaza tawi la kijeshi la Hamas na wanamgambo wake kua ni marufuku,na kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati.

Akitathmini ushindi wao katika uwanja wa mapigano,msemaji wa Hamas Sami Abou Zouhri amesema tunanukuu:”wapalastina wanashuhudia kukombolewa kwa mara ya pili Gaza na kuutakasa safari hii na mahaini ,baada ya kuwatimua walowezi wa kiyahudi.”Mwisho wa kumnukuu.

Mapigano yameenea hadi Ukingo wa magharibi ambako dazeni kadhaa ya wanaharakati wa Hamas wamekamatwa na vikosi vitiifu kwa Fatah.Ofisi ya shirika linaloungwa mkono na Hamas imetiwa moto huko Ramallah katika wakati ambapo huko Beitlaham (Jerusalem) watu wasiojulikana wamelitia moto gari la kiongozi mmoja wa kidini kutoka chama cha Hamas.