1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano ya ukeketaji yanafanane na ya Ukimwi

5 Juni 2019

Wanaharakati wa masuala ya wanawake wametaka harakati za kupambana na ukeketaji dhidi ya wanawake zifanane na zile za kupambana na Ukimwi duniani. Wanawake hao wamekuatana Vancouver, Canada.

https://p.dw.com/p/3Ju5t
Stephanie Sinclair - Gewinnerin des Anja Niedringhauspreis 2017
Picha: IWMF/Stephanie Sinclair

Wanaharakati wa masuala ya wanawake wanaokutana mjini Vancouver, Canada, kwenye mkutano mkubwa kabisa wa masuala ya usawa wa kijinsia wamesema mapambano dhidi ya ukeketaji kwa wanawake yanatakiwa kupewa kipaumbele kimataifa sawa na hatua zinazochukuliwa katika vita dhidi ya Ukimwi. 

Wanaharakati hawa wamefikia hatua ya kutoa mwito kama huu kufuatia wasiwasi wa kuendelea kwa visa vya mila hii mbaya ya ukeketaji duniani, kuliko ilivyodhaniwa.

Taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonyesha takriban wasichana na wanawake milioni 200 wameathirika na ukeketaji duniani kote, lakini baadhi ya wanaharakati wamesema idadi hii inalishusha mno tatizo hilo, kwa kuwa inapingana na ukweli kuhusu kusambaa kwa ukeketaji, lakini pia inawatenga watoto na wanawake wengine.

Simbabwe Farfell Coffee Estate, Chipinge | Ernte
Wanawake wengi ni waathiria wakubwa wa ukeketaji dunianiPicha: DW/P. Musvanhiri

Makisio hayo ya Umoja wa Mataifa yanayotokana na taarifa za ukeketaji kwenye nchi 30, nyingi zikiwa za barani Afrika, wakati wanaharakati katika mkutano huo uliopewa jina "Women Deliver" wakisema kuna tafiti ama ushahidi wa hadithi zinazotolewa na wahanga unaoonyesha ukeketaji umefanyika katika mataifa mengine zaidi ya 30.

Wanaharakati wanasema hawapuuzi harakati za kukabiliana na Ukimwi.

Mkurugenzi wa shirika la wanaharakati wa haki za wanawake la Equality Now la nchini Marekani, Shelby Quast amesema wana uhakika kwamba matukio hayo yanatokea kwenye maeneo mengine, ambayo amesema ni aina nyingine ya udhibiti wa mwili wa mwanamke lakini pia mwanamke mwenyewe.

Wamesema Umoja wa Mataifa umeyaacha mataifa kama Georgia, Urusi, Oman, Sri Lanka, Iran, India, Pakistan, Malaysia, Thailand na Singapore.

Shirika la misaada la nchini Uingereza la kupambana na ukeketaji  linakadiria ufadhili wa kimataifa kwenye tatizo hilo lilifikia karibu dola milioni 200 kati ya mwaka 2018 na 2021, ikilinganishwa na Ukimwi, ambao kwa mwaka 2017 pekee, kulitolewa dola bilioni 20 kwa ajili ya waathirika takriban milioni 37.

Mwasisi wa shirika hilo Julia Lalla-Maharajh ameuambia wakfu wa Reuters kwamba hawana nia ya kupuuzia juhudi hizo, bali wanataka kujifunza, huku wakitoa mwito wa kuimarishwa kwa mchakato wa ukusanyaji wa taarifa ili kufanyika kwa tathmini ya tatizo hilo kimataifa na kuandaa mpango wa kukabiliana nalo.

Mkutano huo wa Deliver Women 2019, umekutanisha wajumbe 8,000 kutoka mataifa 165. Masuala mahsusi yanayojadiliwa yanahusiana na kuwawezesha wanawake lakini pia mabadiliko kwenye sera zihusuzo afya, haki na maisha bora kwa wasichana na wanawake.