1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano ya Jeshi la Congo na wanamgambo yawauwa watu 20

12 Julai 2021

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hali ya wasiwasi inazidi kuripotiwa katika eneo la Minembwe kufuatia mapambano yanayoendelea huko tangu Jumamosi kati ya jeshi la Congo FARDC na makundi ya wanamgambo wa Gumino na Twirwaneho kutoka kabila la Banyamulenge, na upande mwingine kati ya wanamgambo Maï-maï na wanamgambo wa kabila hilo.

https://p.dw.com/p/3wMMT

Mapambano makali yametokea katika baadhi ya vijiji vya pembezoni mwa Minembwe kama vile Kakenge, Runundu na Ilundu tangu Jumamosi asubuhi, na sasa yanaendelea k katika vijiji vingine vya nyanda za wilaya ya Fizi kati ya wanamgambo wa Mai-Mai na wanamgambo wa muungano wa makundi ya Gumino na Twirwaneho.

Jeshi limesema watu wasiopungua ishirini wamepoteza maisha katika mapambano hayo makali.


Katika taarifa yake, jeshi la Congo FARDC linasema kuwa mapambano ya Jumamosi yalijiri baada ya ngome zake kushambuliwa na makundi ya kikabila tiifu kwa kanali Michel Makanîka, ambaye ni afisa wa zamani aliyeasi jeshi la Congo takriban  miaka miwili iliyopita, akidai sasa kupigania masilahi ya jamii yake Banyamulenge, akihisi kuwa inaathirika kutokana na ukosefu wa usalama katika eneo hilo. 


Watu mbali mbali walioshuhudia  wanasema kuwa Jumamosi wanamgambo hao walidhibiti baadhi ya maeneo karibu na uwanja mdogo wa ndege wa Minembwe kabla ya kufukuzwa na jeshi hadi ndani ya milima, na jeshi lika fanikiwa kudhibiti baadhi ya vijiji pembezoni mwa Minembwe.

DRK Symbolbild FARDC
Picha: Alain Wandimoyi/AFP

FARDC yaapa kuwadhibiti wanamgambo


Msemaji wa operesheni za jeshi la FARDC zinazoitwa Sukola yapili, kapiteni Dieudonné Kasereka, anasisitiza kuwa jeshi la Congo lita hakikisha kwamba linarejesha na kudumisha utulivu huko  Minembwe na katika baadhi ya maeneo yanayokaliwa na wanambambo wa mirengo yote.

Mapambano hayo yalisababisha wakaazi wa vijiji vingi kukimbilia msituni, ijapokuwa huko waliko kimbilia pia kunafanyika mapambano mengine kati ya makundi ya wanamgambo Mai-Mai kutoka makabila mengine upande huo na wanamgambo wanaotetea kabila la banyamulenge.

Wiki iliopita, tume ya umoja wa mataifa ya kusimamia  amani nchini Congo Monusco imeahidi katika taarifa yake kuongeza juhudi zake na kushirikiana na jeshi la FARDC katika ulinzi wa vijiji vya Muranvia napia vijiji kadhaa vya Minembwe.