1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maonyesho ya kimataifa ya Vitabu yamefunguliwa rasmi Frankfurt, Ujerumani.

Erasto Mbwana5 Oktoba 2004

Maonyesho ya vitabu, ambayo ni makubwa kuliko yote duniani, yamefunguliwa rasmi muda mfupi uliopita mjini Frankfurt na Kansela wa Ujerumani, Gerhard Schröder na Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Amr Mussa. Kauli mbiyu ya maonyesho ya mwaka huu ni nchi za Kiarabu. Nchi 17 kati ya 22 za Umoja wa Nchi za Kiarabu zinawakilishwa na Wandishi vitabu wa Kiarabu zaidi ya 200 wanashiriki katika Maonyesho hayo.

https://p.dw.com/p/CHiM
Kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani.
Kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani.Picha: AP

Sherehe rasmi za ufunguzi, licha ya kuhudhuriwa na watu kadhaa mashuhuri, zinahudhuriwa pia na Wandishi wa vitabu 1,000 miongoni mwao akiwemo Mshindi wa Tunzo la Nobel la Uandishi Fasihi, Günter Grass.

Mwanafasihi Grass, akishirikiana na Peter Rühmkorf, watasoma hadharani riwaya maalumu siku ya Jumamosi.

Waonyeshaji 6,691 kutoka nchi 110, kuanzia kesho Jumatano, wataonyesha vitabu vipatavyo zaidi ya 350,000. Mwaka uliopita walikuwa 6,638. Kwa hiyo idadi yao mwaka huu imeongezeka kwa asili mia moja. Miongoni mwa Waonyeshaji hao 2,809 wanatoka Ujerumani na 3,882 wanatoka nje ya Ujerumani. Waonyeshaji wengi, licha ya Ujerumani, ni Waingereza ambao wana vibanda vipatavyo 900.

Mkurugenzi wa Maonyesho, Volker Neumann, akizungumza na Wandishi wa Habari leo amesema kuwa athari za mashambulio ya kigaidi nchini Marekani ya Septemba 11 miaka mitatu iliyopita zimeanza kutoweka. Wasiwasi mkubwa waliokuwa nao baadhi ya watu kuhusu usalama wao sasa nao pia umeanza kupotea.

Bw. Neumann amesema kuwa nchi za Kiarabu mwaka huu zimechaguliwa kuonyesha machapisho yao kwa sababu Maonyesho yanatambua umuhimu wa mawasiliano ya ndani zaidi ya tamaduni mbalimbali.

Ameongeza kusema kuwa nchi za Kiarabu zinapaswa kupongezwa kwa sababu hazijawazuia baadhi ya Wandishi wa vitabu au kuchuja machapisho yao kwa sababu za kisiasa.

Vyama vya Wayahudi vimelalamika kuwa nchi za Kiarabu hazipaswi kuwa kauli mbiyu kwa sababu misingi ya kidemokrasia katika baadhi ya nchi hizo haifuatwi.

Wandishi wa vitabu kutoka Libya, Moroko, Algeria, Kuwait na Irak nao pia wanawakilishwa katika Maonyesho ya vitabu ya Frankfurt ingawaje nchi zao hazimo katika kundi la Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji na Wauzaji wa vitabu nchini Ujerumani, Dieter Schormann, amesema kuwa vitabu ni muhimu sana kwa wote. Vinachukua jukumu muhimu katika kuendeleza jamii na fikra zao.

Amezungumzia pia kuhusu neema ya kiuchumi inayoweza kupatikana kutokana na biashara ya vitabu.

Amesema kuwa biashara ya vitabu mwaka huu imepata faida ya asili mia nukta saba ikilinganishwa na mwaka wa jana.

Kilele cha Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu mjini Frankfurt hapa Ujerumani kitakuwa Jumapili wakati Mwandishi wa Vitabu kutoka Hungary, Péter Esterházy, atakapotunikiwa tunzo la Amani la Wachapishaji na Wauzaji wa Vitabu nchini Ujerumani katika Kanisa la Mtakatifu Paulo.

Dibaji ya Tunzo inasema, "Wakfu unatambua umuhimu wa amani, utu na maelewano kati ya Watu. Kwa hiyo, anayetunukiwa tunzo hili amefanya makubwa katika sekta za uandishi fasihi, sayansi, utamaduni na kuendeleza amani. Tunzo hutolewa bila ya kujali taifa la mtu, rangi yake, dini yake au hata imani yake."

Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu mjini Frankfurt yanakosolewa kwa ajili ya gharama kubwa za Hoteli na yalitaka kuhamishiwa Munich, Ujerumani. Lakini licha ya wenye Hoteli kuahidi kuwa wangalipunguza bei za malazi, hawajafanya hivyo.

Maonyesho, kwa mara ya kwanza kabisa, mwaka huu yatamalizika siku ya Jumapili badala ya Jumatatu.