Maoni:Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya uhamiaji
29 Juni 2018Baada ya masaa 12 ya mazungumzo viongozi wa Umoja wa Ulaya waliwasilisha mkataba waliofikia juu ya uhamiaji. Ni mabadiliko ambayo yanaelemea zaidi kwenye mrengo mkali wa kulia unaoelekea kuongeza ugumu kuingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya. Bila shaka vyama vinavyopinga wahamiaji vimepata ushindi.
Mgogoro huo unatakiwa kuhamishiwa nje ya mipaka ya Ulaya ambapo vituo vya uchunguzi vitaanzishwa. Vituo hivyo vinatarajiwa kuwaogofya watu wanaotaka kusafiri kutokea Libya na nchi nyingine za Afrika Kaskazini ambapo wahamiaji wa Kiafrika hujaribu hata kuivuka bahari ya Mediterania ili kufika barani Ulaya.
Mkakati huu unafanana na makubaliano yaliyofikiwa na Uturuki katika eneo la Aegean ambako matumaini ya kutokuwa na uwezo wa kuondoka kutoka kwenye visiwa vya Ugiriki yamesababisha kupungua kwa idadi ya watu wanaotafuta hifadhi na pia kwa vitendo vya wahamiaji kuwalipa wafanya biashara haramu wa kusafirisha watu au hata kupanda boti zisizofaa na kuingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya. Vizuizi ndio utaratibu wa siku hadi siku ila hili sio jambo jipya. Jipya hapa ni hatua mbadala za kuwekwa kwa majukwaa ya kikanda ya kuwateremshia wahamiaji.
Umoja wa Ulaya unataka kuimarisha ushirikiano wake na Libya, eneo ambako wahamiaji wanakabiliwa na unyanyasaji na mateso. Walinzi wa pwani ya Libya, tayari wanapokea msaada wa umoja huo na baadaye watawajibika katika kuwadhibiti wahamiaji katika eneo kubwa la bahari ya Mediterania. Lengo lake ni wazi kabisa kwamba watu ambao watajiweka kwenye hatari ya kusafiri baharini moja kwa moja watarejeshwa walikotoka.
Fedha nyingi zitatumika kwenye mkakati huu, usambe sifa za ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika, ambazo matokeo yake yanapaswa kuonekana katika miongo ijayo.
Mkakati huu wa kuwazuia wahamiaji unaweza kuonekana kuwa ni madhubuti, lakini kuhusu njia inayotumiwa na wahamiaji kati ya Libya na Italia, hicho bado ni kitendawili kwa Umoja wa Ulaya. Swali jee, ni nani atakayevijenga vituo vya uchunguzi na vipi hasa ulinzi wake utakavyoshughulikiwa, ni jambo ambalo halielezeki ila kubakia tu na kusubiri kuona yatakayotokea.
Kansela wa Ujerumani? Angela Merkel amefanikisha padogo sana kuhusiana na mgogoro wa kisiasa unaotokota nchini mwake. Ikiwa Ujerumani itawakataa wanaotafuta hifadhi katika mipaka yake kama waziri wake wa mambo ya ndani, Horst Seehofer, anavyotaka, basi Austria itawapeleka hadi Italia wahamiaji hao na kufunga mipaka yake. Bibi Merkel bado hajafikia mkataba wowote wa nchi mbili hizo kuhusu mambo yanavyopaswa kuendelea.
Juu ya yote, idadi ya wahamiaji wanaokuja barani Ulaya imeshuka kwa asilimia 95 hapa ni jinsi ya kuzuia asilimia 5 ya wahamiaji waliobaki wasiweze kuingia barani Ulaya.
Mwandishi: Zainab Aziz/Bernd Riegert
Mhariri: Mohammed Khelef