1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel azuru Uturuki wakati mgumu

Admin.WagnerD3 Februari 2017

Ziara  ya Kansela Angela Merkel Uturuki imekuja katika wakati mgumu ambapo viongozi wa nchi hizo wamelenga kushughulikia baadhi ya matatizo yakiwa katika hali tete na hakukuwa na matumaini ya kujongeleana baina yao.

https://p.dw.com/p/2WuHo
Türkei Treffen Angela Merkel & Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/K. Azher

Ziara  ya Kansela Angela Merkel nchini Uturuki imekuja katika wakati mgumu ambapo viongozi wa nchi hizo wamelenga kushughulikia baadhi ya matatizo yakiwa katika hali tete na hakukuwa na matumaini ya kujongeleana baina ya viongozi hao wawili anaandika Seda Serdar mwandishi wa DW.

Hakuna ziara ya Merkel ilokuwa rahisi nchini humo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.Hata hivyo hii ilikuwa na umuhimu wake kwa Uturuki kutokana na kwamba nchi hiyo inajiandaa kwa kura ya maoni ambayo inaweza kubadili sana utaratibu wa demokrasia uliokuweko tokea jadi.

Bila ya shaka Uturuki ina fungu lake la mapungufu ya demokrasia lakini hatua zilizochukuliwa na serikali kufuatia jaribio la mapinduzi lililoshindwa katika kipindi cha ya kiangazi kilichopita imeyapandisha daraja mapungufu hayo kufikia kiwango ambacho kilikuwa hakijulikani kabla na raia na washirika wa nchi hiyo.

Katika mikutano na waandishi wa habari iliohudhuriwa pia na Rais Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu Binali Yildrim katika nyakati tofauti Kansela Merkel amegusia kijujuu suala la uhuru wa vyombo vya habari na kutenganisha madaraka.

Pia amezungumzia umuhimu wa kuwa na upinzani wa kisiasa katika nchi zinazofuata demokrasia. Kuiangalia hali hiyo kwa mapana kwa kuzingatia mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa,kukamatwa kwa maelfu ya watu au kutimuliwa makazini,kuzimwa kwa sauti za upinzani bila ya shaka hayo hayaonyeshi ukubwa wa hali halisi ilioko nchini humo.

Kuweka wazi njia za mawasiliano

Türkei  Angela Merkel - Binali Yildirim
Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildrim.Picha: Reuters/Ho

Ni hali tete kwa Merkel hususan kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi nchini Ujerumani.Kwa upande mmoja akiwa kama mwakilishi wa maadili ya Ulaya inabidi asimame kidete kumkabili Erdogan.Kwa upande mwengine hawezi kuwa wazi mno kukabiliana na hali hiyo jambo ambalo linaweza kupelekea kusambaratika kwa makubaliano kuhusu wakimbizi kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Suala hilo ni tete kwa Kansela kwani kuweka wazi njia za mawasiliano sio kazi rahisi.Suala la makubaliano hayo kuhusu wakimbizi sio suala pekee nyeti. Kashfa ya DITIB ambapo baadhi ya maimamu wanaofanya kazi na shirika hilo wanatuhumiwa kufanya upepelezi kwa niaba ya serikali ya Uturuki ni suala jengine tata.

Juu ya kwamba Merkel amedai kupatiwa ufafanuzi viongozi wote wawili wa Uturuki wamekwepa kuzungumzia suala hilo hadharani.Jambo hilo litaendelea kusababisha mvutano kati ya nchi hizo mbili.

Licha ya taarifa za kirafiki kuhusu uhusiano wa kihistoria na kifedha kati ya nchi hizo na umuhimu wa kupambana na ugaidi inanaonekana kwamba hivi sasa huko Uturuki kila kitu kinahusu sisitizo juu ya matatatizo na hali ya kutoridhika.

Wakati sio muafaka

Takriban hakuna matamshi ya tija ambayo yanatowa mwanga kwa hatua zinazofuata.Ujumbe pekee ulio wazi uliojitokeza ni kuendelea kuyaweka makubaliano kuhusu wakimbizi kwenye mkondo.

Juu ya kwamba wakati wa kufanyika kwa ziara hii umekosolewa Merkel hakuona kuna tatizo katika kukutana na viongozi wa Uturuki kabla ya kufanyika kwa kura hiyo muhimu ya maoni juu ya mabadiliko ya katiba .

Ni kweli Merkel amekutana pia na vyama vya upinzani CHP na HDP ambapo alishindwa kufanya hivyo wakati wa ziara yake ya mwezi wa Oktoba mwaka 2015 kabla ya uchaguzi mkuu jambo hilo halitokizuwiya chama tawala cha Erdogan cha AKP kuitumia kwa faida yake ziara hii na kuitumia kama mtaji kwa kampeni yake ya kura ya maoni.

Mwandishi : Seda Serdar/Mohamed Dahman

Mhariri :Yusuf Saumu