1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May ajitayarisha kuwa Waziri Mkuu

Admin.WagnerD13 Julai 2016

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya Waziri Mkuu mtarajiwa wa Uingereza Theresa May na juu ya hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa kuhusu bahari ya kusini ya China.

https://p.dw.com/p/1JO8B
Waziri Mkuu mtarajiwa wa Uingereza Theresa May
Waziri Mkuu mtarajiwa wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/C. Furlong

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linaanza kwa kuuliza jee Waziri Mkuu mpya wa Ungereza atakuwa na msimamo wa chuma?

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba mama huyo anatambua vizuri kuwa Uingereza imo katika hatari ya kumegeka. Viongozi katika jiji la London walisahau kuzipima hisia za kusini ya nchi yao-yaani Scotland. Mhariri wa "Neue Osnabrücker"anasema watu wa Scotland wanautaka Umoja wa Ulaya.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba Waziri Mkuu mpya Theresa May ataingia madarakani wakati ambapo Uingereza inakabiliwa na mikanganyiko pia ndani ya vyama vyake vikuu vya kisiasa.

Matukio ya Dallas

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen" anasema yaliyotukia katika mji wa Dallas yanaonyesha jinsi matumizi ya nguvu yanavyoweza kuwa hatari.

Gazeti hilo linasema Mkuu wa polisi katika mji wa Dallas alisema kuwa aliitumia njia ya mwisho,yaani mabavu! Njia hiyo inaweza kuwa sahihi kwa mtazamo wake lakini matokeo yake ni maafa.

Mhariri wa gazeti la "Mannheimer Morgen " anaeleza kuwa polisi nchini Marekani wanasahau kwamba siyo jukumu lao kuwaua wahalifu. Polisi hao wanapaswa kutafautisha kati ya jukumu lao na la lile la wanajeshi. Lengo la mwanajeshi ni kumwangamiza adui ili kumshinda.

China yashindwa mahakamani

Mahakama maalumu ya kimataifa jana ilitoa hukumu juu ya Bahari ya kusini ya China.Kwa mujibu wa mahakama hiyo China haina haki ya kuwa mmiliki wa bahari hiyo. Lakini China imeipinga hukumu hiyo.

Mazoezi ya kijeshi kwenye bahari ya China Kusini
Mazoezi ya kijeshi kwenye bahari ya China KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/Xinhua/Z. Chunming

Mhariri wa "Rheinpfalz" anasema China inajenga hoja kwa matendo katika bahari ya kusini ya nchi hiyo.Inayafukia matumbawe na pia inajenga kituo cha kijeshi. Ndiyo kusema hukumu iliyotolewa jana na mahakama maalumu ya kimataifa haitazizuia hatua hizo. China inashikilia kwamba Bahari hiyo ni mali yake.

Jambo baya zaidi ni kwamba nchi nyingine zinazopakana na bahari hiyo hazina nguvu mbele ya China. Mhariri wa "Rheipfalz" anasema China ina nguvu kubwa. Ni kweli kwamba mara moja moja Marekani inapeleka ndege zake za kijeshi kwenye anga ya bahari ya kusini ya China.
Lakini hakuna anaeweza kufirikia kwamba Marekani inataka kukabiliana kijeshi na China.

Gazeti la "Märkische Oderzeitung" linasema tatizo kubwa lililopo ni kukosekana kwa taifa lenye nguvu la kuitekeleza hukumu kama hiyo iliyotolewa dhidi ya China.Ni kweli kwamba Marekani inapeleka manowari na ndege za kivita katika sehemu hiyo lakini haiwezi kuizuia mipango ya China.Hata hivyo hukumu hiyo ni pigo kwa China.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef