1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washtushwa juu ya ubakaji mjini Cologne

Admin.WagnerD6 Januari 2016

Wahariri wanazungumzia juu ya mrengo mpya wa siasa nchini Poland na juu ya mikasa ya ubakaji katika mji wa Cologne iliyowashtusha viongozi wa nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1HZ8C
Picha: picture-alliance/dpa/L.Szymanski

Wahariri hao pia wanatoa maoni juu ya Saudi Arabia baada ya utawala wa nchi hiyo kuwanyonga watu zaidi ya 40 wakati mmoja.

Kuhusu Poland gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeiutung" linasema nchi hiyo inayakiuka maadili ya kidemokrasia na msingi wa utawala wa kisheria wa Umoja wa Ulaya.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Poland inaenda kinyume na maadili hayo kwa kuchukua hatua za kuyarudisha nyuma mageuzi yanayowafiki na misingi ya Umoja wa Ulaya.

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linasema itakuwa sahihi kwa Umoja wa Ulaya kuingilia kati nchini Poland na kusisitiza umuhimu wa nchi hiyo kufuata utaratibu wa utawala wa kisheria. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema Umoja wa Ulaya unapaswa pia kuzitazama nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.

Mikasa ya ubakaji mjini Cologne

Idadi kubwa ya wanawake walibakwa katika mkesha wa mwaka mpya katika mji huo. Lakini kadhia hiyo imeleta utatanishi kutokana wageni kuhusishwa na uhalifu huo.

Maandamano ya kupinga uhalifu wa ubakaji mjini Köln
Maandamano ya kupinga uhalifu wa ubakaji mjini KölnPicha: Reuters/W. Rattay

Kwa mfano gazeti la "Märkische" linapiga vijembe kwa kusema ,mgeni anaefuata sheria, atakuwa na haki ya kuishi nchini Ujerumani bila ya kujali nasaba yake.Lakini yule anaekiuka sheria, lazima afukuzwe nchini!

Mhariri wa gazeti la "Die Welt" anauliza kwa nini imechukua muda mrefu ili kujua kilichotokea? Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba wahusika , polisi,baraza la mji na serikali kuu wamechelewa kujua kwa uhakika juu ya uhalifu uliotendeka katika mji wa Cologne kwa sababu hiyo ni hali mpya mpya kabisa. Lakini yaliyotokea katika mji huo ni mbiu ya mgambo. Maana yake ni kwamba walinzi wa amani ya mji wanapaswa kutiliwa maanani zaidi.


Gazeti la masuala ya kibiashara "Handelsblatt" linazungumzia juu ya Saudi Arabia. Mhariri wa gazeti hilo anaanza kwa kuuliza ,Jee inawezekana, kwa Ujerumani na nchi nyingine za magharibi kuendelea kufanya biashara na utawala wa Saudi Arabia usiotaka kujifunza lolote? Mhariri wa gazeti anasema hakuna jibu la swali; ni kwa kiasi gani inawezekana kufanya biashara na kuendeleza uhusiano na tawala zenye matatizo.

Anaeleza kuwa haitakuwa sahihi wakati wote kuweka vikwazo,kwa wale wasiokubaliana na maadili ya magharibi .Lakini anasema pia siyo sahihi kufuata ruwaza ya kizamani kwamba, biashara hatimaye inaleta mageuzi, ingawa wakati huo huo haki za binadamu zinapuuzwa.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef