1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Putin wakutana

Admin.WagnerD29 Septemba 2015

Wahariri wanazungumzia juu ya mkutano wa Marais Obama na Putin na madai kwamba waziri wa ulinzi wa Ujerumani aligushi tasnifu yake ya uzamifu. Pia wanatoa maoni juu ya hali ya nchini Afghnaistan.

https://p.dw.com/p/1GfDn
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Freie Presse" linazungumzia juu ya mkutano baina ya Marais wa Marekani Barack Obama na wa Urusi ,Vladimir Putin ngwazoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba Marais hao wamezungumzia juu ya mgogoro wa Syria na dhima ya Rais wa nchi hiyo,al -Assad katika kuutatua mgogoro huo .Mhariri huyo anaitaka Marekani ijihadhari, la sivyo itaupoteza ushawishi wake katika Mashariki ya Kati. Anasema ili kumtelekeza al-Assad, Putin anaweza kudai malipo makubwa sana kutoka kwa Marekani.


Naye mhariri wa gazeti la "Der neue Tag" anasema ni vizuri kwamba Marais Obama na Putin wamekutana. Lakini hakuna matumaini makubwa. Mhariri huyo anaeleza kuwa Marais wa Marekani na Urusi wanapaswa kuwa na shabaha ya pamoja, yaani kuwazuia magaidi wanaoitwa dola la kiislamu, na kuwashinda. Lakini nini kinapasa kufanyika baada ya hapo, hakuna sera ya pamoja.


Mhariri wa gazeti la "Rheinpfalz" anahoji kwamba alieibuka mshindi, baada ya mkutano wa marais hao wawili ni bwana Putin, kutokana na ukweli kwamba Rais Obama alikubali kukutana naye kwenye Umoja wa Mataifa.

Hali ya Afghanistan inazidi kuwa mbaya

Mhariri wa gazeti la "Volkssitimme" anatoa maoni juu ya uwezo wa Taliban wa kuendelea kufanya mashambulio makubwa nchini humo. Anaeleza kwamba hali ya usalama imezidi kuwa mbaya sana baada ya majeshi ya kimataifa kuondoka nchini Afghanistan.

Serikali ya Afghanistan haina uwezo wa kuwadhibiti Taliban.Hayo yamethibitika kutokana na shambulio kubwa lililofanywa katika mji wa Kundus. Wapiganaji wa Taliban hata wamethubutu kuipandisha bendera yao kati kati ya mji huo.Pana hatari ya serikali ya Afghanistan kulipoteza jimbo lote la kaskazini.

Mazungumzo baina ya serikali ya Afghanistan na Taliban bado ni jambo lililosimama mbali sana. Lakini hiyo ndiyo ingelikuwa njia pekee ya kuepusha maafa ya vita.

Waziri mwengine wa ulinzi wa Ujerumani akabiliwa na tuhuma
Kwa mara nyingine yametolewa madai juu ya waziri mwengine wa Ujerumani juu ya kughushi tasnifu. Tuhuma hizo zimeelekezwa kwa waziri wa ulinzi, Ursula von der Leyen.

Deutschland Ursula von der Leyen
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Gazeti la "Nordwest" linasema watu wanakumbuka yaliyotokea kwa mawaziri waliokabiliwa na tuhuma kama hizo hapo awali. Aliekuwa waziri wa ulinzi,Karl-Theodor zu Guttenberg, na aliekuwa waziri wa elimu Shavan. Wote walikanusha vikali hapo mwanzoni. Lakini mwishowe tasnifu zao zilibatilishwa.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman