Maoni ya wahariri
4 Desemba 2014Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatoa maoni juu ya uamuzi wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wa kuitisha uchaguzi wa bunge mapema.Mhariri wa gazeti hilo anasema kufanyika uchaguzi huo hakutaifanya hali ya kisiasa iwe nzuri nchini Israel, na badala yake patakuwa na hofu juu ya serikali ya Israel kudhibitiwa na watu wenye siasa kali. Na ndiyo kusema ,suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati, halitapatikana .Ndoto ya kuundwa dola ya Wapalestina itatoweka.
Ukraine yashauriwa kutojiunga na NATO kwanza
Mhariri wa gazeti la "Rhein-Necker "anazishauri nchi za Nato ,kutoihimiza Ukraine ijiunge na mfungamano wa kijeshi wa NATO. Mhariri huyo anasema halitakuwa shauri la busara kwa Rais Petro Poroshenko wa Ukraine kutoa maombi ya kujiunga na NATO sasa. Mhariri huyo anahoji kwamba mazungumzo yanayoendelea sasa baina ya nchi za magharibi na Putin bado ni magumu.
Na gaazeti la "Süddeutsche" linasema Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg amesema jambo sahihi kabisa kwamba kila nchi inao uhuru wa kuwania kujiunga na mfungamano wa kijeshi wa Nato.Kauli hiyo inapokelewa kwa matumaini makubwa nchini Ukraine.Hata hivyo kauli ya kweli inapasa kuwa, marafikii wa Ukraine mnaweza kutoa maombi ya kujiunga na Nato, lakini haina maana kwamba wanachama wote wa jumuiya hiyo ya kijeshi watakubaliana. Mhariri anasema njia pekee ya kuikabili Urusi kwa ufanisi ni kuonyesha misuli sambamba na kufanya mazungumzo.
Putin aubatilisha mradi wa bomba la nishati
Rais Vladimir Putin wa Urusi ameyatikisa masoko ya nishati kwa kuitangaza hatua ya kuubatilisha mradi wa dola Bilioni 20 wa bomba la mkondo wa kusini, wa kupeleka mafuta na gesi katika nchi za Ulaya magharibi. Lengo la Putin ni kuepuka kulipitishia bomba hilo katika ardhi ya Ukraine. Na badala yake litapitia Uturuki.
Juu ya uamuzi wa Rais Putin gazeti la "Südkurier linasema Rais Putin amekosea mahesabu. Mhariri anasema viongozi wanaweza kudanganya lakini hesabu zinawasuta. Sasa Putin anayapata malipo ya mpango wake wa kibabe wa kutaka kuijenga Urusi kubwa .Sarafu ya nchi yake inaanguka thamani, na nchi yake inatumbukia katika mdodoro wa uchumi.
Putin ameekosea, kwani nchi za magharibi zina njia kadhaa za kuishinikiza Urusi na kuizuia mipango ya kibeberu ya Rais Putin. Hata hivyo nchi za magharibi zinapaswa kuicha wazi njia ya mazungumzo.
Mwandishi:Mtullya abdu.Deutsche Zeitungen
Mhariri: Yusuf Saumu