1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya6 Novemba 2013

Pamoja na masuala mengine wahariri leo wanazungumzia juu ya madai kwamba Uingereza pia imekuwa inafanya upelelezi nchini Ujerumani kutokea kwenye ubalozi wake mjini Berlin.

https://p.dw.com/p/1ADAJ
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters

Wahariri hao pia wanatoa maoni juu ya mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Juu ya tuhuma za Uingereza kuzipeleleza taasisi za serikali ya Ujerumani gazeti la "Nürberger Nachrichten" limetoa mwito wa kuwepo subira katika maoni yake.

Gazeti la"Nürnberger Nachrichten" linasema utakuwa ushauri mzuri kuvuta subira juu ya suala hilo. Mhariri wa gazeti hilo anasema mashirika ya ujasusi ya nchi za magharibi, ikiwa pamoja na ya Ujerumani hayajengi usalama zaidi kwa kupelelezana. Ni kinyume chake-yanasababisha wasiwasi tu.

Gazeti la "Nürberger Nachrichten" linasema mchezo wa kupelelezana unakihatarisha kile ambacho kinapaswa kulindwa na mashirika hayo-yaani demokrasia.Ni vizuri kwamba nyendo hizo zinafichuliwa, lakini itakuwa vizuri zaidi ikiwa zitakomeshwa. "Ubalozi wa Marekani wa mjini Berlin umezifunga mashine zake za udukuzi .Hiyo ni hatua muhimu."

Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Gazeti la "Badische"linatoa maoni juu ya mazungumzo kuhusu Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.Gazeti hilo linasema kwamba litakuwa shauri zuri kwa Umoja wa Ulaya kuicha milango yake wazi kwa ajili ya Uturuki. Mhariri wa gazeti hilo amehoji kwamba watu wanaweza kubishana juu ya ruwaya,yaani kigezo cha uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya. Lakini wote wanakubaliana kwamba Uturuki ni nchi muhimu barani Ulaya, kutokana mahala ilipo kijografia na kutokana na uzito wake wa kisiasa.

Ujerumani yanalumiwa kwa mafanikio yake !

Mhariri wa "Landeszeitung" anazungumzia juu ya lawama zilizotolewa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Ujerumani.Umoja wa Ulaya unailaumu Ujerumani kwa kufikia ziada ya kiwango kikubwa katika biashara ya nje. Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anasema, lawama kama hizo bora zielekezwe katika nchi zinazokata pua ili kuunga wajihi.

Mhariri huyo anasema licha ya kuwa mfano mzuri,Ujerumani inatiwa hatiani.Kosa, ni kufikia ziada kubwa katika biashara yake ya nje.Halmashauri ya Umoja wa Ulaya hata imefikia hatua ya kutishia kuichukulia Ujerumani hatua za kinidhamu.

Mhariri huyo amesema mambo yatakuwa kichwa chini miguu juu kuiadhibu nchi inayoupanga vizuri mustakabal wake badala ya kuwakaripia wale wanaotumia mikakati ya kizamani ya kulimbikiza madeni ili kuendesha uchumi. Nchi hizo zinapaswa, kuambiwa na Umaja wa Ulaya, zifanye mageuzi badala ya kuitumia njia hiyo ya kizamani. Kwa hivyo, lawama zinazotolewa na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya juu ya Ujerumani, ni upuuzi mtupu.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo