1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya22 Oktoba 2013

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya ustawi wa uchumi nchini Ujerumani, mkwaruzano baina ya Ufaransa na Marekani kutokana na kashfa ya udukuzi na juu ya mkasa wa Askofu wa dayosisi ya Limburg.

https://p.dw.com/p/1A3yM
Rais Francois Hollande wa Ufaransa
Rais Francois Hollande wa UfaransaPicha: Reuters

Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linazungumzia juu ya dhima ya vyama vya upinzani katika Bunge la Ujerumani. Mhariri wa gazeti hilo anasema ikiwa serikali ya mseto itaundwa baina ya vyama vikuu,vya CDU,SPD na chama cha CSU upinzani katika bunge la Ujerumani utabakia kuwa kiduchu. Sababu ni kwamba vyama vya upinzani havitakuwa na viti vya kutosha vya kuwawezesha kuidhibiti serikali kwa uthabiti.

Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linasema, katika demokrasia panahitajika taratibu za kuyadhibiti mamlaka ya serikali kwa kuwepo upinzani thabiti.Lakini utaratibu huo sasa upo mashakani,na ndiyo sababu kwamba vyama vikuu vitakavyounda serikali vijaribu kuziimarisha haki za pande za wachache bungeni.

Askofu wa Limburg

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaizungumzia kashfa inayomkabili Askofu wa dayosisi ya Limburg nchini Ujerumani, Tebarzt van -Elst. Pamoja na mambo mengine ,Askofu huyo anakabiliwa na madai ya ubadhirifu.Lakini mhariri wa gazeti hilo anaungalia mkasa huo kwa kina kirefu zaidi. Na anasema kuwa mjadala juu ya suala la Askofu wa dayosisi ya Limburg una kina kirefu. Kwani mambo yanayohusika katika suala hilo hayaishii katika ubadhirifu wa Askofu huyo. Mambo ya msingi yanapaswa kuzingatiwa .Kwa mfano, jee Kanisa Katoliki lina utajiri wa kiasi gani? Mkasa wa dayosisi ya Limburg umedokeza usiri uliopo juu ya fedha za Kanisa.

Uchumi wa Ujerumani

Gazeti la "Südwest Presse"linauangalia uchumi wa Ujerumani kwa furaha kubwa kutokana na ustawi unaotarajiwa mwakani.Hata hivyo gazeti hilo linatahadharisha kwa kusema kwamba ustawi zaidi, nafasi zaidi za ajira na mapato zaidi ya kodi yanaweza kuwa mashakani kutokana na ugeugeu wa bei za malighafi na kutokana na hali ya utashi ,nje ya Ujerumani inayoweza kubadilika. Ujerumani haina udhibiti juu ya hali kama hizo.Lakini Ujerumani inao udhibiti juu ya masuala ya kodi na mabadiliko ya sera ya nishati.

Ufaransa na Marekani zakwaruzana

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatoa maoni juu ya mkwaruzano uliopo baina ya Ufaransa na Marekani kuhusu madai ya udukuzi uliofanywa na shirika la ujasusi la Marekani,NSA. Mhariri wa gazeti hilo anasema mpaka sasa suala hilo halijaibua mawimbi makubwa nchini Ufaransa. Lakini mambo yanaweza kubadilika.
Hoja kwamba upelelezi uliofanywa na shirika la ujasusi la Marekani, NSA unahusu magaidi na wahalifu wengine haina mashiko kutokana na kiwango kikubwa cha data zilizohusika.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman