1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

Abdu Said Mtullya30 Oktoba 2012

Wahariri wa magazeti leo wanatoa maoni yao juu ya kimbunga Sandy ,mgogoro wa Syria na mvutano baina ya Ugiriki na pande tatu zinazoitwa Troika. Pia wanamzungumzia aliekuwa waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi

https://p.dw.com/p/16ZOS
Kimbunga "Sandy" kilichoikumba Marekani
Kimbunga "Sandy" kilichoikumba MarekaniPicha: TIMOTHY A. CLARY/AFP/Getty Images

Juu ya kimbunga Sandy nchini Marekani gazeti la "Nurnberger" linasema yumkini mtu anaweza kufikiri ni ufidhuli kusema kuwa kimbunga hicho kinaweza kuamua nani atakuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais nchini Marekani. Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha juu ya uchaguzi mkuu wa nchini Ujerumani mnamo mwaka wa 2002. Kansela aliekuwa madarakani wakati huo Gerhard Schröder hakuwa na matumaini makubwa. Lakini ghafla kutokana na maafa ya mafuriko, aliyoyakabili vizuri, mambo yalibadilika kwa manufaa yake. Kwa hivyo ikiwa Obama atathibiti kuwa mdhibiti imara wa hali ya hatari,iliyosababishwa na kimbunga Sandy, huenda upepo wa neema ukavumia upande wake.

Mhariri wa gazeti la"Der neue Tag" pia anazungumzia juu ya kimbunga Sandy, na anasema Marekani inao uzoefu wa kuzikabili hali za maafa kama vile matetemeko ya ardhi, mafuriko, mioto ya misituni na vimbunga.Lakini licha ya kuwa majanga ya asili, wananchi wanaziangalia hali kama hizo kwa macho makali. Kwani wakati wa majanga hayo ndipo wanapoibuka mashujaa au magoigoi. Jee nani ananufaika na hali za maafa.Ni swali la kubeza lakini, hali hizo za hatari ni sehemu ya kampeni za uchaguzi.

Gazeti la "Südwest Presse" linatupia macho matukio ya nchini Syria. Mhariri wa gazeti hilo anasema jumuiya ya kimataifa inaweza kuwa na matumaini ya kurejea amani nchini Syria kutokana na jambo moja tu, Kwamba pande zinazopigana siku moja zitachoka na kulazimika kuziweka silaha chini.

Mpaka sasa pande tatu zinazoitwa Troika hazijatoa ripoti juu ya Ugiriki,ambayo ni muhimu sana kwa nchi hiyo. Kwani ripoti hiyo ndiyo itakayoamua iwapo Ugiriki itapatiwa msaada mwingine wa fedha. Kwa nini ripoti hiyo inachelewa kutolewa.? Mhariri wa "Ludwigsburger Kreiszeitung" anaeleza kuwa yumkini pande tatu,zinazofanya mazungumzo na Ugiriki hazijakubaliana juu ya kuikabili Ugiriki kuhusu masharti iliyopewa.Lakini anasema ukweli unabakia pale pale kwamba walipa kodi ndio wanaolibeba zigo.Jee ni mpaka lini viongozi wataendelea kusubiri?

Gazeti la "Die Welt" limeandika juu ya aliekuwa Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi aliesema kuwa anakusudia kurejea katika harakati za kisiasa. Mhariri wa gazeti hilo anasema Italia itakuwa katika hali nzuri ikiwa vyama vya kisiasa vya mrengo wa kati kulia vitaunda mhimili utakaomweka Berlusconi nje kabisa-mfungamano wa kihafidhina ambao hautamhitaji Berlusconi asilani.Italia inastahili kuwa na mambo mazuri zaidi kuliko kuendelea na tamthilia.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen:

Mhariri:Yusuf Saumu